Watoto wahanga wakuu wa maafa ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i14110-watoto_wahanga_wakuu_wa_maafa_ya_syria
Watoto ndio wahanga wakuu wa mgogoro wa Syria. Hii ni kutokana na kuwa, licha ya kuwa watoto hao hawana nafasi yoyote ile katika kuenea vita nchini Syria, lakini wao wamekuwa ndio wahanga wakuu wa mafaa ya nchi hiyo kuliko tabaka jingine lolote lile.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 28, 2016 02:28 UTC
  • Watoto wahanga wakuu wa maafa ya Syria

Watoto ndio wahanga wakuu wa mgogoro wa Syria. Hii ni kutokana na kuwa, licha ya kuwa watoto hao hawana nafasi yoyote ile katika kuenea vita nchini Syria, lakini wao wamekuwa ndio wahanga wakuu wa mafaa ya nchi hiyo kuliko tabaka jingine lolote lile.

 Anthony Lake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF ameelezea tena wasiwasi mkubwa alionao kuhusiana na hali ya kibinadamu katika mji wa Halab huko Syria na kutangaza kwamba, kuanzia mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka huu, zaidi ya watoto laki moja wamekumbwa na matatizo ya vita katika maeneo ya mashariki mwa mji huo na kwamba, zaidi ya watoto elfu 35 wamelazimika kuyahama makazi yao na kuelekea katika maeneo ya Magharibi.

Syria kama zilivyo aghlabu ya nchi za Kiarabu, katika miezi ya awali ya mwaka 2011 ilikumbwa na wimbi la malalamiko dhidi ya serikali. Hata hivyo Syria ina tofauti mbili muhimu na nchi nyingine za Kiarabu zilizokumbwa na wimbi la malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali. Tofauti hizo zina uhusiano na hali ya kijiografia ya Syria pamoja na nafasi ya kisiasa ya nchi hiyo katika eneo la magharibi mwa Asia.

Hii ndio taswira ya miji mingi ya Syria

Syria ina mpaka wa pamoja na utawala wa Kizayuni wa Israel, Iraq, Jordan, Uturuki na Lebanon ambapo kila moja kati yake ina umuhimu mkubwa kwa ajili ya madola makubwa kieneo na nje ya eneo hili la Mashariki ya Kati. Syria ina nafasi muhimu ya kisiasa katika eneo la magharibi mwa Asia kama ilivyo nafasi yake ya kijiografia. 

Hii ni kutokana na kuwa, Syria ni moja ya mihimili ya muqawama katika Mashariki ya Kati ambao unapinga ubeberu na kile kinachojukana kama mapatano. Sababu hizi mbili zilikuwa kisingizio tosha cha kubadilisha sauti ya malalamiko dhidi ya serikali huko Syria na kwa uingiliaji wa madola yanayopinga mhimili wa muqawama hususan Saudi Arabia, Marekani, Uingereza, Ufaransa, Uturuki, Qatar na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuifanya kuwa vita vya kimataifa kwa kuyatumia makundi ya kigaidi.

Huu ni mwezi wa 65 ukiwa unaelekea kumalizika tangu kuanza vita hivyo ambapo akthari ya mikoa na miji ya Syria haijabakia isipokuwa magofu na taswira ya majengo kubomolewa. Miundombinu ya kijamii na ya miji imeteketezwa huku zaidi ya Wasyria milioni 11 wakilazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Aidha maelfu ya watu wameuawa na kujeruhiwa katika vita vya Syria. Kimsingi tunaweza kusema katika sentensi moja kwamba, katika akthari ya miji ya Syria hakuna athari ya maisha.

Mtoto wa Kisyria katika moja ya kambi za wakimbizi Syria

Nukta ya kusikitisha ni kwamba, athari ya vita nchini Syria inahusiana zaidi na watoto. Kwa maana kwamba, watoto wa nchi hiyo ndio walioathiriwa zaidi na vita hivyo. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, watoto hao hawakuwa na nafasi yoyote ile si ya kuanzisha au hata kueneza vita hivyo.  Kutokana tu kwamba, ni Wasyria, watoto hao wamejipata kwamba, leo na kesho yao inaelekea kupotea bure bilashi.

Hatima na majaaliwa ya watoto wa Syria hii leo ni kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo, kufukiwa na vifusi vinavyotokana na makombora ya magaidi yanayolenga nyumba za watu, kutaabika na njaa na kuteseka kwa kiu, kukumbwa na maradhi na kutopata huduma muhimu za kitiba. Chambilecho,  Anthony Lake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF ni kuwa, watoto wa Syria wamekuwa wakiishi maisha yaliyotawaliwa na woga na wahaka mkubwa.

Hii ikiwa ni leo ya watoto wa Syria; lakini kesho yao nayo haiko salama; kwani imegubikwa na wimbi la matatizo ya kiroho na kisaikolojia yaliyotokana na vita , maisha bila ya kuwa na msimamizi wa familia, kutokuwa na mahala pa maana pa kujihifadhi, kukosa nafasi ya kupata elimu, kupatwa na vilema vya maisha na msururu wa matatizo mengine.

Swali la kujiuliza ni hili kwamba, katika zama ambazo nara na kaulimbiu za haki za binadamu zinapigwa, maripota maalumu wanaainishwa kwa ajili ya kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi tofauti na demokrasia inapigiwa upatu, je,  ni kwa nini watoto wa Syria na Yemen ambao wanataabika katika vita ambavyo vimepandikizwa na hawa hawa wanaodai kuwa ni watetezi wa haki za binadamu pamoja na washirika hao, hawana hisa katika nara na madai haya yanayotolewa?