Hasira za Marekani na Israel kwa uamuzi wa UNESCO kuhusu Quds
Uamuzi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) wa kusisitiza kuwa Mayahudi hawana uhusiano wowote ule na Masjidul Aqsa, (Kibla cha Kwanza cha Waislamu) wala mji wa Quds, umewahamakisha sana viongozi wa utawala wa Kizayuni na Marekani
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amedhihirisha hamaki zake kwa kudai kuwa uamuzi huo wa UNESCO wa kupinga vitendo vya Israel katika mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas na Msikiti wa al Aqsa, eti ni uamuzi ulkiochukuliwa kinyume cha sheria na kwamba Israel haitojali maamuzi ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa bali itaendelea kupora ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Naye Mark Toner, kaimu wa msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema kuwa nchi yake inapinga vikali uamuzi huo wa UNESCO wa kulaani vitendo vya Israel huko Quds na Masjidul Aqswa na kudai kuwa eti hatua hiyo itaongeza matatizo katika eneo la Mashariki ya Kati. Siku ya Alkhamisi, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) lilipasisha muswada uliosisitiza kuwa, hakuna uhusiano wowote wa kihistoria, kidini na wala wa kiutamaduni baina ya Mayahudi na maeneo matakatifu katika mji wa Quds ukiwemo Msikiti wa al Aqsa. Nchi 24 wanachama wa shirika hilo walipiga kura ya kuunga mkono haki hiyo ya taifa la Palestina na kuzishinda nchi sita zilizopinga, huku nchi 26 nyingine zikijizuia kupiga kura.
Muswada huo wa UNESCO si tu umelaani vitendo vya Wazayuni vya kupotosha asili ya kihistoria ya Quds, lakini pia umesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unapaswa kuacha kujitanua na kufanya vitendo vya ukatili katika maeneo ya watu wengine. Muswada huo umesisitiza pia kuwa, Israel lazima iheshimu maazimio na matamko ya shirika hilo la kimataifa. Hayo yamejiri katika hali ambayo utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea na njama zake za kuudhibiti kikamilifu mji mtakatifu wa Quds na njama hizo zimekuwepo tangu Israel ilipouvamia mji huo mtukufu. Hadi sasa ni baadhi tu ya maeneo ya mashariki mwa mji huo ndiyo yaliyobakia mikononi mwa Wapalestina, baada ya Israel kuteka maeneo mengine yote.
Mwaka 2014 utawala wa Kizayuni ulianzisha mpango wa kuteka na kupora pole pole maeneo ya mashariki mwa mji wa Quds na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Vitendo hivyo vya Wazayuni vinakinzana kikamilifu na maazimio ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la 478 la Baraza la Usalama la umoja huo ambalo linatamka wazi kuwa walimwengu wana wajibu wa kupinga na kukataa hatua yoyote ile ya Israel ya kujiingiza katika masuala ya mji wa Quds, kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika mji huo na pia njama za Israel za kujaribu kuuangisha mji huo mtakatifu na maeneo mengine ya Palestina inayoyakalia kwa mabavu.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa kufanikiwa Palestina kupata uanachama katika Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kumezitia kwenye mtihani mkubwa siasa za kupenda kujitanua za utawala wa Kizayuni na kuziongezea mbinde juhudi za kimataifa za kupigania haki za Wapalestina. Kwa hakika misimamo ya mara kwa mara ya UNESCO ya kupinga vitendo vya kidhalimu vya Israel katika mji wa Baytul Muqaddas, mji ambao walimwengu wanauangalia kwa hisia kali sana, inaonesha ni jinsi gani walimwengu wanavyozidi kuchukizwa na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina. Si hayo tu, lakini pia uamuzi huu wa hivi sasa wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) unaitilia mkazo jamii ya kimataifa ichukue hatua za haraka na za kweli za kuhakikisha kuwa, utawala wa Kizayuni unakomesha mara moja jinai zake huko Palestina.