Russia yaionya Marekani dhidi ya kuwatoa magaidi Iraq hadi Syria
Russia imeionya Marekani dhidi ya kuwafurusha wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh kutoka Iraq hadi Syria, katika mashambulizi yake ya kuukomboa mji wa Mosul, kaskazini mwa Iraq.
Valery Gerasimov, kamanda mwandamizi wa jeshi la Russia amesema kuna haja ya kuwaangamiza magaidi wa kitakfiri katika operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul, ili kuepuka hatari ya magenge hayo ya kigaidi kukimbilia Syria.
Mashambulizi ya kila upande ya jeshi la Iraq kwa kushirikiana na harakati za wanchi kwa ajili ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa wanachama wa genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh yalianza rasmi Jumatatu iliyopita.
Rais Putin wa Russia amesema kuwa, operesheni za kuukomboa mji wa Mosul ni hatua muhimu sana katika njia ya kupambana na ugaidi.
Rais Putin ameyasema hayo katika mazungumzo ya simu na Haider al-Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq ambapo ameonyesha matarajio kuona jeshi la nchi hiyo likifanikiwa kuukomboa mji huo kutoka kwa wanachama wa kundi hatari la kigaidi la Daesh kama ilivyoainishwa.
Mji wa Mosul unakaliwa kwa mabavu na wanachama wa kundi hilo la Kiwahabi la Daesh tangu tarehe 10 mwezi Juni mwaka 2014 na kuufanya kuwa makao makuu yake.