Jeshi la Syria laendeleza operesheni za kijeshi dhidi ya magaidi
Kikosi cha anga cha Syria kimefanya mashambulio makubwa dhidi ya ngome za kundi la kigaidi linalojulikana kama Jaish al-Fat'h katika maeneo ya kaskazini mwa mji wa Hama ulioko magharibi mwa nchi hiyo.
Duru za kijeshi za Syria zinaarifu kwamba, mashambulio hayo ya anga ya jeshi yamepelekea makumi ya magaidi kuangamia na wengine wengi kujeruhiwa.
Aidha jeshi la Syria limefanya mashambulio dhidi ya ngome za kundi la kigaidi la Jab'hat al Nusra (Fat'h Sham) katika kambi ya Nazihin na katika maeneo mengine ya kusini mwa Syria na kulisababishia hasara kubwa kundi hilo la kigaidi. Aidha idadi kadhaa ya magaidi wa kundi hilo wameangamizwa katika operesheni hiyo ya kijeshi ya jeshi la Syria,
Katika upande mwingine, vikosi vya jeshi la Syria vimeshambulia maficho ya magaidi wa Jabhat al-Nusra na makundi yanayofungamana na kundi hilo katika mji wa Homs magharibi mwa nchi hiyo. Viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa kundi hilo wanaripotiwa kuuawa katika operesheni hiyo.
Wakati huo huo, Talal al-Barazi, Gavana wa mji wa Homs ameashiria jitihada za jeshi la Syria na waitifaki wake kwa ajili ya kuyakomboa baadhi ya maeneo yaliyo jirani na medani ya gesi katika maeneo ya mashariki mwa mji huo na kusema kuwa, mapigano kati ya pande mbili yanaendelea katika eneo hilo.
Habari kutoka nchini Syria zinaeleza kuwa, jeshi la nchi hiyo limeendelea kupata mafanikio na kusonga mbele katika maeneo mengi yaliyokuwa yakidhibitiwa na magaidi.