Makumi ya mamluki wa Saudia waangamizwa katika shambulizi Yemen
Makumi ya mamluki wa Saudi Arabia wanaomuunga mkono rais mtoro wa Yemen Abdu Rab Mansur Hadi wameuawa katika shambulizi la bomu lililofanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, katika mji bandari wa Aden, kusini mwa nchi.
Kanali ya televisheni ya Press TV imeripoti kuwa, shambulio hilo la bomu limetokea katika kituo cha mamluki hao wilayani al-Arish, kaskazini mashariki mwa mji wa Aden.
Inaarifiwa kuwa, gaidi aliyekuwa amejifunga mabomu alijiripua katika mkusanyiko wa mamluki hao wa Saudia, walipokuwa wamepanga foleni kupokea mishahara yao na kwamba 49 miongoni mwao wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
Tarehe 10 Disemba pia, kulitokea shambulio jingine kama hiyo lililofanywa na magaidi wa kitakfiri wa Daesh katika kambi ya kijeshi mjini Aden, ambapo wanamgambo 48 wanaomuungana mkono Hadi waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hali ya kibinadamu nchini Yemen inaelezwa kuzidi kuwa mbaya kufuatia hujuma ya kijeshi ya Saudi Arabia na washirika wake na kwamba kuna haja ya kuchukuliwa hatua za haraka za kukabiliana na hali mbaya inayowasulubu wananchi wa nchi hiyo. Hivi karibuni Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF ulisema kuwa watoto wasiopungua 462,000 wanateseka kutokana na hali mbaya mno ya lishe duni na wengine milioni mbili na laki mbili wanahitaji matunzo ya haraka.
Mashambulio hayo yamekuwa yakizilenga skuli, hospitali, makaazi ya raia, misikiti, barabara, masoko na kambi za wakimbizi na kuua maelfu ya raia wasio na hatia wa Yemen. Zaidi ya watu 11,400 wameshauawa hadi sasa katika hujuma ya kinyama ya Saudia dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu.
