Magaidi 76 wa Daesh waangamizwa katika mji wa Mosul, Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i22753-magaidi_76_wa_daesh_waangamizwa_katika_mji_wa_mosul_iraq
Vyombo vya usalama nchini Iraq vimetangaza habari ya kuuawa makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul ulioko kaskazini mwa nchi.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jan 03, 2017 10:21 UTC
  • Magaidi 76 wa Daesh waangamizwa katika mji wa Mosul, Iraq

Vyombo vya usalama nchini Iraq vimetangaza habari ya kuuawa makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul ulioko kaskazini mwa nchi.

Polisi ya Federali ya Iraq imetangaza leo Jumanne kuwa, wanachama 50 wa Daesh wameuawa katika operesheni zilizofanyika katika miji ya Misaq na Shaima, huku wengine 13 wakiuawa katika operesheni nyingine tofauti iliyofanyika katika mji wa Sana’ah.

Taarifa ya kitengo hicho cha polisi ya Iraq imeongeza kuwa, wanachama wengine zaidi ya 10 wa kundi la wakufurishaji la Daesh wameangamizwa katika maeneo mengine yanayopakana na Mosul. Hata hivyo imeripotiwa kuwa, raia 11 wameuawa katika shambulizi la roketi la Daesh katika eneo la makazi ya watu, mashariki mwa mji huo.

Operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul, Iraq

Abdul-Amir Rashid Yar-Allah, Kamanda Mkuu wa Operesheni za Kijeshi Mkoani Nineveh amesema kuwa, vikosi vya Iraq vimefanikiwa kusambaratisha ngome muhimu za Daesh, hususan katika barabara inayoiunganisha Mosul na mji wa Tal Afar katika mkoa huo. Ameongeza kuwa, vikosi vya Iraq vimefanikiwa kukomboa kijiji cha al-Karama, katika operesheni hizo.

Ikumbukwe kuwa, operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul, makao makuu ya mkoa wa Nainawa nchini Iraq kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh, ilianza tarehe 17 Oktoba mwaka uliomalizika kwa amri ya Waziri Mkuu wa Iraq, Haydar al Abadi. Mji huo wa kistarajia umekuwa chini ya udhibiti wa matakfiri wa Daesh tokea mwaka 2014.