Polisi Bahrain washambulia shule na kufyatulia wanafunzi mabomu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i23293-polisi_bahrain_washambulia_shule_na_kufyatulia_wanafunzi_mabomu
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekosoa vikali hatua ya maafisa usalama wa Aal-Khalifa nchini Bahrain kushambulia shule moja na kuwafyatulia wanafunzi mabomu ya kutoa machozi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 12, 2017 00:16 UTC
  • Polisi Bahrain washambulia shule na kufyatulia wanafunzi mabomu

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekosoa vikali hatua ya maafisa usalama wa Aal-Khalifa nchini Bahrain kushambulia shule moja na kuwafyatulia wanafunzi mabomu ya kutoa machozi.

Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la SALAM for Democracy and Human Rights, maafisa wa polisi wa Bahrain jana Jumatano walivamia shule moja katika kisiwa cha Sitra, yapata kilomita 5 kusini mwa mji mkuu, Manama na kuwarushia mabomu ya kutoa machozi wanafunzi walikuwa wakishiriki maandamano ya amani ya kupinga utawala wa Aal-Khalifa.

Mwanafunzi mmoja amejeruhiwa vibaya jicho lake baada ya polisi wa Bahrain kumfyatulia usoni bomu la kutoa machozi.

Mwanafunzi wa Bahrain aliyejeruhiwa kwa bomu la kutoa machozi

Katika tukio nyingine tofauti, maafisa usalama wa Manama jana Jumatano walifanya msako mkali katika majengo ya makazi ya watu katika kijiji cha Nuwaidrat ambapo watu wanne walikamatwa na askari wa Bahrain na kupelekwa kusikojulikana.

Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa Aal-Khalifa tangu Februari mwaka 2011. Matakwa makuu ya wananchi hao ni kuwepo utawala wa kisheria, kukomeshwa ubaguzi wa kimadhehebu, kufanyika mageuzi ya kisiasa na kuheshimiwa haki za binadamu.

Aidha wamekuwa wakiandamana wakionyesha uungaji mkono wao kwa mwanazuoni mashuhuri wa madhehebu ya Shia, Ayatullah Sheikh Issa Qassem, anayehesabiwa kuwa kiongozi wa kiroho wa vuguvugu la mapinduzi ya wananchi wa Bahrain.