Jan 16, 2017 03:52 UTC
  • Iran yalaani mauaji ya wanaharakati Bahrain, upinzani waitisha maandamano nchi nzima

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali hatua ya utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain ya kuwanyonga wanaharakati watatu wa nchi hiyo kwa madai bandia ya kuhusika na shambulizi la kigaidi la mwaka 2014.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi amesema kuwa, kuendelea kuwekewa mbinyo na mashinikizo wapinzani wa Bahrain kutaitumbukiza nchi hiyo ya Kiarabu katika kinamasi na mkwamo wa kisiasa.

Amesema taasisi za kimataifa za kutetea haki za binadamu pamoja na asasi zisizo za kiserikali kote duniani zimebainisha namna ambavyo hakukuwepo haki na uadilifu katika mchakato mzima wa kusikiliza kesi dhidi ya wanaharakati hao.

Wanaharakati walionyongwa na utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, kitendo hicho cha kikatili cha utawala wa Aal-Khalifa  kwa mara nyingine tena kimeudhihirishia ulimwengu kuwa, watawala wa Manama hawawezi kutumia njia za amani na kisheria kuupatia ufumbuzi mgogoro wa aina yoyote na kuwaonya wajiandae kwa balaa na mzozo mkubwa usio na mfano wa kisiasa unaonukia.

Huku hayo yakiarifiwa, vyama vya upinzani nchini Bahrain kikiwemo cha Kiislamu cha al-Wefaq vimetoa wito wa kufanyika maandamano ya nchi nzima ya kulaani kitendo cha kikatili cha kunyongwa wanaharakati hao. Vyama vingine vya upinzani vilivyotoa wito wa kufanyika maandamano ya nchi nzima ya kulaani mauaji hayo ya kikatili ya vijana wanaharakati wa Kishia nchini Bahrain ni pamoja na Muungano wa Vijana wa Mapinduzi ya Februari 14, Youth of Diraz na Islamic Action Society.  

Polisi wa Bahrain wakiwafyatulia mabomu ya kutoa machozi waandamanaji jana Jumapili

Hapo jana Agnes Callamard, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya mauaji ya kiholela na udikteta alisema wanaharakati hao wameuawa pasina kuwepo ushahidi juu ya madai wanayolimbikiziwa. Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, utawala wa Manama umewanyonga wanaharakati Abbas al-Samea, Ali al-Singace na Sami Mushaima baada ya kuteswa, kudhalilishwa na kuhukumiwa pasina ushahidi wa kutosha.  

Tags