Jan 20, 2017 07:36 UTC
  • Amnesty yaitaka Bahrain iache kuwanyonga wafungwa wa kisiasa

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema Bahrain inaelekea kutumbukia katika mgogoro wa haki za binaadamu na inapaswa kusitisha mara moja hukumu ya kunyongwa wafungwa wengine wawili wa kisiasa nchini huo.

Mahakama ya Bahrain mwaka 2014 iliwahukumu kunyongwa wanaharakati wawili wa kisiasa, Mohammad Ramadhani na Hussein Ali Musa kwa madai yasiyo na msingi. Hivi sasa imedokezwa kuwa utawala wa ukoo wa Aal Khalifa unajitayarisha kutekeleza hukumu ya kifo dhidi ya wafungwa hao wawili ambao wamenyimwa haki zao za kisheria wakiwa jela. Aidha taarifa zinasema kuwa, wafungwa hao wawili wameteswa kwa muda mrefu sana na hatimaye wakalazmishwa kukiri makosa ambayo hawakuyafanya.

Jumapili iliyopita, utawala wa Manama uliwanyonga wanaharakati Abbas al-Samea, Ali al-Singace na Sami Mushaima baada ya kuteswa, kudhalilishwa na kuhukumiwa pasina ushahidi wowote wa kuhusika na vitendo walivyotuhumiwa kufanya.    

Vijana wanaharakati wa kisiasa Bahrain walionyongwa

Tokea mwezi Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia harakati ya mwamko wa Kiislamu ambapo wananchi wanataka kuwa na haki ya kuwachagua viongozi wao na kuwepo usawa na uadilifu katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.

Utawala Bahrain ambao ni muitifaki mkubwa wa Marekani na Uingereza, umekuwa ukikandamiza maandamano ya amani ya wananchi na tayari idadi kubwa ya watu wameshauawa, mamia kujeruhiwa na wengine wengi kushikiliwa kidhulma magerezani.

Tags