Ushirikiano wa Ujerumani na Saudi Arabia katika vita dhidi ya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i28500-ushirikiano_wa_ujerumani_na_saudi_arabia_katika_vita_dhidi_ya_yemen
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye siku ya Jumapili alifanya safari nchini Saudi Arabia, ameitaka nchi hiyo kusimamisha mashambulio yake dhidi ya taifa la Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 01, 2017 08:54 UTC
  • Ushirikiano wa Ujerumani na Saudi Arabia katika vita dhidi ya Yemen

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye siku ya Jumapili alifanya safari nchini Saudi Arabia, ameitaka nchi hiyo kusimamisha mashambulio yake dhidi ya taifa la Yemen.

Akizungumza huko Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, Bi. Merkel amesema kuwa anaamini kwamba mgogoro wa Yemen unapaswa kutatuliwa kwa njia za kidiplomasia kwa usimamizi wa Umoja wa Mataifa na kuwa hadhani kwamba mgogoro huo unaweza kutatuliwa kijeshi.

Madai ya kansela wa Ujerumani kuhusiana na udharura wa kusimamishwa uvamizi wa Saudia huko Yemen na kutafutwa njia za kisiasa kwa ajili ya kusimamisha vita vya kichokozi dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu yanatolewa katika hali ambayo Ujerumani ni mshirika mkubwa wa Saudia anayeiuzia silaha za kisasa na kuwapa mafunzo ya kijeshi askari wake wanaoendelea kutenda jinai na mauaji ya kinyama dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen. Kwa hakika Angela Merkel anatekeleza siasa za kindumakuwili kuhusiana na uchokozi wa Saudia huko Yemen ambapo hivi sasa tunashuhudia kuimarika ushirikiano wa kijeshi kati ya Berlin na Riyadh ambapo mwaka uliopita wa 2016 pekee Ujerumani iliiuzia Saudia silaha za kisasa zenye thamani ya zaidi ya dola nusu bilioni.

Angela Merkel akiwa na mwenyeji wake Mflame Salman

Wakati huohuo nchi hiyo ya Magharibi mwezi uliopita wa Aprili ilithibitisha kuiuzia Imarati silaha za dola milioni 134, jambo ambalo limekabiliwa na ukosoaji mkubwa wa ndani na nje ya nchi hiyo. Chama cha rangi ya kibichi cha Ujerumani ni moja ya makundi yanayokosoa vikali uuzwaji wa silaha za nchi hiyo kwa Saudi Arabia ambayo inakiuka wazi haki za binadamu ndani na nje ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa msemaji wa chama hicho, badala ya serikali ya Ujerumani kusimamisha uuzaji silaha kwa nchi zote zinazoshiriki katika vita vya Yemen, imekiuka sheria na kanuni zote za uuzaji nje silaha za nchi hiyo. Katika miongo kadhaa iliyopita Ujerumani imekuwa ikijaribu kuwa na nafasi muhimu katika soko la uuzaji silaha Mashariki ya Kati, silaha ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuchochea mivutano na machafuko katika eneo na wakati huohuo kurefusha umri wa watawala madikteta wa Kiarabu. Kimsingi Ujerumani inaiuzia silaha Saudi Arabia kwa malengo mawili.

Uharibifu unaofanywa na silaha za Saudia Yemen

La kwanza ni kuwa kutokana na muelekeo wa hivi sasa wa uchumi wake, Ujerumani inakusudia kutafuta vyanzo vingine vya kujipatia fedha za kigeni na kuandaa nafasi za ajira kwa vijana wake, kupitia sekta ya mauzo ya silaha nje ya nchi. Lengo la pili ni kwamba nchi hiyo inakusudia kulinda uchumi wake kwa kuimarisha mauzo ya bidhaa zake nje ya nchi zikiwemo silaha. Kwa kufanya hivyo nchi hiyo ya Magharibi bila shaka inashiriki katika juhudi za kulinda tawala mbovu na tegemezi za Kiarabu Mashariki ya Kati, ambazo zinashirikiana na nchi za Magharibi katika kukandamiza harakati za wananchi wanaopigania haki zao za msingi katika nchi hizo na hasa Saudia. Ni kwa kutilia maanani ukweli huo ndio maana nchi za Magharibi ikiwemo Ujerumani zikawa zinafumbia macho ukiukaji wa wazi na mkubwa wa haki za binadamu unaotekelezwa katika nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na hasa Suadia, pamoja na jinai za kutisha zinazofanywa na nchi hiyo huko Yemen kupitia mashambulio yake ya miezi 25 sasa dhidi ya taifa hilo.

Watoto wa Yemen wanaoathirika kutokana na uchokozi wa Saudia dhidi ya nchi yao

Suala hilo linaweka wazi undumakuwili unaofanywa na nchi za Magharibi kuhusiana na suala zima la haki za binadamu. Nchi hizo licha ya kuwepo ripoti chungu nzima zinazotolewa na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu dhidi ya Saudia kuhusiana na mauaji yake dhidi ya raia wa Yemen na vilevile kulaaniwa mara kadhaa nchi hiyo kuhusiana na ukiukaji wake wa wazi wa haki za binadamu lakini bado nchi hizo za Magharibi zinadumisha uhusiano wa karibu wa kijeshi na nchi hiyo ya Kiarabu.