Wayemen waikosoa Imarati kwa kuanzisha mrengo wa wanamgambo nchini mwao
Viongozi wa kisiasa wa maeneo ya kusini mwa Yemen wanaoishi mjini Sana'a, mji mkuu wa Yemen wamekosoa vikali hatua ya serikali ya Imarati ya kuanzisha mrengo wa wanamgambo ndani ya ardhi yao kwa lengo la kuigawa Yemen na kudhibiti maeneo ya kusini mwa taifa hilo.
Hatua ya Imarati ya kuanzisha mrengo huo imekuja kufuatia kuongezeka tofauti nyingi baina yake na Saudia kuhusiana na Yemen. Kwa mujibu wa duru za habari nchini Yemen, mrengo huo wa wanamgambo uliopewa jina la 'I'laamiyyat Tarikh Aden' una mafungamano na Aydarus al Zubaidi, mkuu wa mkoa wa zamani wa Aden aliyeondolewa madarakani hivi karibuni na Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu wadhifa huo na kukimbia nchi.
Hivi karibuni pia maelfu ya Wayemen walifanya maandamano makubwa katika kulalamikia siasa za Abdrabbuh Mansur Hadi na washirika wake yaani Saudia za kuukabidhi mkoa wa Aden kwa wapiganaji wenye mafungamano na genge hatari la al-Qaidah mjini Aden. Itafahamika kuwa, Mansur Hadi alichukua hatua ya kumfuta kazi Aydarus al Zubaidi ambaye anaonekana kuungwa mkono na Imarat, hatua ambayo ililalamikiwa vikali na raia wa taifa hilo.
Wayemen wanamtaja Abdrabbuh Mansur Hadi kuwa chanzo cha mgogoro na kuongezeka machafuko nchini humo huku akijikita katika kuunda makundi ya kigaidi yanayopata himaya ima kutoka Saudia au Imarati. Saudia kwa kushirikiana na Marekani, Israel na Uingereza ilianzisha mashambulizi yake ya kichokozi dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 kwa lengo la kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wao huyo, mashambulizi ambayo hata hivyo yameshindwa kufikia malengo yake, ghairi ya kusababisha maafa kwa raia wa kawaida wa Yemen.