Misri yakanusha kuingilia masuala ya ndani ya Sudan
Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri amekanusha madai kwamba Cairo inaingilia masuala ya ndani ya Sudan.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa pamoja na Kansela wa Austria, Christian Kern, Rais Abdel Fattah el Sisi amejibu tuhuma zilizotolewa na Khartoum dhidi ya Misri na kusema kuwa, Cairo haingilii kabisa masuala ya jirani yake Sudan.
Amesema, siasa za Misiri ni kuheshimu sheria za kimataifa na kujiepusha kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Rais wa Misri aidha amesema, nchi yake haifanyi njama dhidi ya nchi yoyote, na inajiepusha kikamilifu na vitendo viovu vya aina hiyo.
Majibu hayo ya Rais wa Misri yametolewa katika hali ambayo uhusiano wa nchi yake na Sudan umeingia katika matatizo kutokana na mambo mengi ikiwemo mzozo wa kugombania eneo la pembe tatu la Halaib lililoko katika mpaka wa nchi hizo mbili na uungaji mkono wa Sudan kwa Ethiopia katika suala zima la ujenzi wa bwawa la al Nahdha kwa kutumia maji ya mto Nile.
Hivi karibuni taasisi rasmi za Misri zilidai kuwa magaidi wanaofanya mauaji nchini humo wanapata mafunzo katika ardhi ya Sudan madai ambayo yameuingiza mzozo wa nchi hizo mbili katika hali mbaya zaidi.