Jeshi la Iraq laangamiza magaidi zaidi ya 75 wa Daesh
Jeshi la Iraq limetangaza kuwa limefanikiwa kuangamiza wanachama 75 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika operesheni tatu kaskazini mwa nchi, katika mikoa ya Salahuddin, Kirkuk na Nineveh.
Jabbar al-Mamouri, kamanda mwandamizi wa kundi linalounga mkono jeshi la Iraq ameiambia kanali ya televisheni ya satalaiti ya al-Sumaria kuwa, operesheni ya kwanza iliyofanyika karibu na mji wa Tikrit imeangamiza magaidi 40 wa Daesh wakiwemo makamanda wao 6. Miongoni mwa makamanda hao ni Abu Qa’qa al-Misri, Abu Osama al-Ansari na Talhah al-Araqi.
Habari zinasema kuwa, magaidi 21 wa Daesh wameuawa katika operesheni nyingine ya jeshi la Iraq karibu na Mlima Sinjar, mkoani Nineveh. Wakati huo huo, madaesh 14 wameripotiwa kuuawa katika mkoa wa Kirkuk, kusini magharibi mwa nchi.
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa watu 670 wameuawa katika machafuko na mashambulizi ya kigaidi nchini Iraq kwenye mwezi uliopita wa Februari pekee. Takwimu zilizotolewa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq (UNAMI) zimeonesha kuwa Wairaqi 670 wameuawa mwezi uliopita wa Februari na wengine 1290 kujeruhiwa katika mashambulizi ya kigaidi. Takwimu hizo zimeonesha kuwa, raia waliouawa ni 410 na wengine 1050 wamejeruhiwa. Umoja wa Mataifa umesema Wairaqi 849 waliuawa nchini Iraq mwezi wa Januari mwaka huu na wengine 1450 kujeruhuwa.
Kundi la kigaidi la Daesh linaloungwa mkono na Saudi Arabia, Uturuki na Qatar limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika maeneo ya umma na kuua idadi kubwa ya raia wasio na hatia nchini Iraq.