Chokochoko mpya za Marekani dhidi ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i31156-chokochoko_mpya_za_marekani_dhidi_ya_syria
Sambamba na kuanza mchezo mpya wa White House dhidi ya Syria, vyombo vya habari vya nchi hiyo vimetangaza habari ya ndege za kivita za Marekani kushambulia mji wa Deir ez-Zor mashariki mwa nchi hiyo ambapo zimeua makumi ya wanawake na watoto katika eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 30, 2017 13:33 UTC

Sambamba na kuanza mchezo mpya wa White House dhidi ya Syria, vyombo vya habari vya nchi hiyo vimetangaza habari ya ndege za kivita za Marekani kushambulia mji wa Deir ez-Zor mashariki mwa nchi hiyo ambapo zimeua makumi ya wanawake na watoto katika eneo hilo.

Habari zinasema kuwa watu wasiopungua 40 waliuawa katika shambulio hilo la kinyama lililotekelezwa na Wamarekani siku ya Jumatano. Siku ya Jumanne pia ndege hizo zilishambulia eneo jingine la Mayadeen katika mkoa huohuo wa Deir ez-Zor ambapo raia wengine 42 wasio na hatia waliuawa. Marekani imekuwa ikifanya mashambulio kama hayo dhidi ya raia wa Syria bila ya kuwa na kibali cha Umoja wa Mataifa wala kuratibu mashambulio hayo kwa ushirikiano na serikali ya Damascus kwa kisingizio eti cha kupambana na magaidi wa Daesh. Jambo lisilo na shaka ni kuwa mashambulio hayo ya Marekani dhidi ya raia wa kawaida wa Syria yamekuwa yakifanyika kwa ushirikiano wa kundi hilo la kigaidi. Kwa maneno mengine ni kuwa Marekani imekuwa ikishirikiana na magaidi wa Daesh katika kushambulia na kuwaua kinyama wananchi wa Syria. Hata kama Marekani imetangaza kuwa iko kijeshi nchini Syria kwa lengo la kupambana na magaidi wa Daesh lakini ni wazi kuwa lengo la nchi hiyo ni kuudhoofisha mrengo halisi unaopambana na magaidi hao watenda jinai.

Shambulio la kemikali linalodaiwa kufanywa Khan Sheikhun

Mashambulio ya kijeshi yanayotekelezwa na Marekani katika maeneo yanayodhibitiwa na jeshi la Syria na washirika wake ambao wako mstari wa mbele wa kupambana na magaidi ni ishara ya wazi kuwa Marekani inayatumia makundi hayo ya kigaidi kudhamini maslahi yake huko Syria. Madai mapya ambayo yametolewa na Marekani dhidi ya Syria kuhusiana na matumizi ya silaha za kemikali yanakumbusha madai kama hayo yasiyo na msingi yaliyotolewa na nchi hiyo dhidi ya Damascus kuhusiana na mashambulio ya kemikali ya tarehe 4 Aprili mwaka huu huko Khan Sheikhun katika mkoa wa Idlib. Shambulio hilo ambalo hadi leo halijathibitishwa muhisika wake lilitumiwa na Rais mpenda vita Dolald Trump wa Marekani kushambulia kwa makombora kituo cha anga cha Shayrat nchini Syria. Shambulio hilo lilitekelezwa katika hali ambayo hadi sasa hakuna nyaraka zozote zinazothibitisha kwamba ni serikali ya Syria ndiyo ilihusika na shambulio hilo la kemikali.

Moja ya jinai zinazotekelezwa na magidi wa Daesh nchini Syria kwa ushirikiano wa Marekani

Wakati huohuo Seymour Hershi mwandishi na mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Marekani amesema kuwa Wamarekani walitekeleza shambulio hilo dhidi ya Syria hali ya kuwa walikuwa wakijua vyema kwamba hakuna shambulio lolote kama hilo la kemikali lililotekelezwa katika eneo lililotajwa bali jeshi la Syria lilishambulia ghala la silaha la Daesh katika eneo hilo. Mchezo wa Khan Sheikhun unathibitisha kwamba Marekani imeanzisha mchezo mwingine kama huo ili kuandaa utangulizi wa kushambuliwa tena Syria kwa madai yasiyo na msingi. Kuhusu suala hilo Konstantin Kosachev, mkuu wa kamati ya uhusiano wa kigeni ya seneti ya Russia anasema kuwa chokochoko mpya zilizoanzishwa na Marekani dhidi ya Syria hazifai kabisa. Amesema hata kama Marekani wana habari kuhusiana na shambulio jingine 'la kemikali' nchini Syria lakini haifanyi lolote kuzuia shambulio hilo bali inamlenga moja kwa moja Rais Bashar Asad wa nchi hiyo au kutumia jambo hilo kama utangulizi wa kutekeleza mashambulio mangine ya kichokozi dhidi ya nchi hiyo.

Marekani ikivurumisha makombora yake katika kituo cha anga cha Shayra, Syria

Madai yasiyo na msingi ya Marekani kwamba Syria inajiandaa kutekeleza shambulio la kemikali katika ardhi ya nchi hiyo ni mchezo mbya na hatari ambao uneweza kutumiwa vibaya na magadi kwa lengo la kutekeleza jinai dhidi ya taifa la Syria na kihsha kuelekeza lawama za jinai hiyo dhidi ya serikali ya Damascus. Ni kutokana na suala hilo ndipo Syria, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia zikaionya vikali Marekani dhidi ya kuchukua hatua nyingine mpya ya kijeshi dhidi ya Syria. Akizungumza hapo siku ya Jamatano, Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alisisitiza kwamba Moscow itatoa jibu kali dhidi ya hatua yoyote ya kichochezi ya Marekani dhidi ya Syria.