Aug 06, 2017 03:09 UTC
  • Amnesty International: Saudia isiwanyonge wapinzani 14 wa serikali ya Riyadh

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka Saudi Arabia itupilie mbali uamuzi wa kuwanyonga wapinzani 14 wa serikali ya nchi hiyo waliolazimishwa kukiri makosa ambayo hawajafanya kutokana na mateso na manyanyaso.

Amnesty International imetangaza kuwa, watuhumiwa hao wamelazimishwa kukiri makosa chini ya mateso na kwamba suala hilo linakosesha thamani matamshi ya kukiri makosa yaliyotolewa baada ya mateso na manyanyaso.

Taarifa ya shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu imesema, kutokana na kutozingatiwa haki na uadilifu, kesi ya watuhumiwa hao inapaswa kurudiwa tena kwa kusheshimiwa sheria za kimataifa. 

Amnesty International pia imetoa wito wa kufanyika uchunguzi huru na wa wazi kuhusu mwenendo wa kuwalazimisha watuhumiwa kukiri makosa ambayo hawajafanya chini ya mateso na manyanyaso nchini Saudi Arabia.

Shirika la Amnesty International lenye makao yake London nchini Uingereza linasema kuwa, takwimu za kunyongwa watu Saudi Arabia ndizo za juu zaidi duniani na kwamba hadi kufikia sasa katika mwaka huu wa 2017 pekee watu 66 wamenyongwa nchini humo.

Wasaudia wakiandamana kupinga dhulma na uaonevu wa serikali

Wakazi wa maeneo ya mashariki mwa Saudia ambao aghlabu yao ni Waislamu wa madhehebu ya Shia wamekuwa wakifanya maandamano ya amani kudai haki na mgao wa kiadilifu wa utajiri wa nchi hiyo. Maandamano hayo yamekabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa jeshi la Saudi Arabia na vijana na wanaharakati wengi wa masuala ya kijamii na haki za binadamu wameuawa, wamehukuwa kifo au vifungo vya miaka mingi jela.   

Tags