Nasrallah: Saudia ilimshinikiza Hariri ajiuzulu kama Waziri Mkuu wa Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i36200-nasrallah_saudia_ilimshinikiza_hariri_ajiuzulu_kama_waziri_mkuu_wa_lebanon
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah amesema, kujiuzulu Saad Hariri kama Waziri Mkuu wa Lebanon ni uamuzi ambao ulilazimishwa na utawala wa Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 06, 2017 05:51 UTC
  • Nasrallah: Saudia ilimshinikiza Hariri ajiuzulu kama Waziri Mkuu wa Lebanon

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah amesema, kujiuzulu Saad Hariri kama Waziri Mkuu wa Lebanon ni uamuzi ambao ulilazimishwa na utawala wa Saudi Arabia.

Nasrullah aliyasema hayo jana jioni ya Jumapili katika hotuba aliyoitoa mjini Beirut, mji mkuu wa Lebanon baada ya kujiuzulu Hariri. Ameongeza kuwa, Hariri alitakiwa afike Riyadh na hapo wakuu wa Saudia wakamlazimisha kujiuzulu na wakamuandikia barua yake ya kujiuzulu watakavyo wao.

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema kujiuzulu Hariri kunaonyesha namna Saudi Arabia inavyoingilia masuala ya ndani ya Lebanon.

Sayyid Hassan Nasrullah amesema Hizbullah haikutaka Hariri ajiuzulu na kwamba kujiuzulu kwake kunakiuka mamlaka ya kujitawala, izza na heshima ya Lebanon.

Sayyid Nasrullah ameashiria suala la kwenda sambamba kujiuzulu kwa Hariri na  kukamatwa wanawafalme kadhaa nchini Saudia na kusema: "Suali linaloulizwa hapa ni hili kuwa, je, tunaweza kutizama kujiuzulu Hariri kama sehemu ya vita na malumbano ndani ya Saudia na eneo la Mashariki ya Kati?

Saad Hariri

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza udharura wa kulinda amani na utulivu wa Lebanon na kuongeza kuwa: "Nawaaambia Walebanon wasiwe na wasiwasi na wote waende kwa mujibu wa mantiki na akili na wasitafakari kurejea katika mazingira ya zamani ya malumbano ya kikaumu na kimadhehebu."

Vilevile ameashiria madai ya kuwepo njama za kutaka kumuua kabla hajajiuzulu na kusema: "Moja ya sababu ya kanali ya Saudia ya Al Arabiya  kudai kuwa kulikuwa na njama za kumuua Saad Hariri ni kumzuia kurejea Lebanon."

Katibu Mkuu wa Hizbullah ameashiria pia uvumi wa Israel kuanzisha vita dhidi ya Lebanon baada ya kujiuzulu Hariri na kusema: "Waisraeli hawataingia katika vita na Lebanon isipokuwa tu wawe na yakini watapata ushindi mutlaki katika vita hivyo."