Abbas amtahadharisha Trump kuhusu hatari ya kuhamishia ubalozi Quds
Kiongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amewasiliana na viongozi kadhaa wa kimataifa akiwemo Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis akiwahimiza kupinga mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kutaka kuhamishia ubalozi wa nchi hiyo katika mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
Msemaji wa serikali ya Palestina, Nabil Abu Rudeina amesema Mahmoud Abbas amewahimiza Papa Francis, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Rais wa Russia Vladimir Putin na Mfalme wa Jordan kusimama kidete na kuzuia mpango wa Rais wa Marekani wa kutaka kuhamishia obalozi wa nchi hiyo huko Quds (Jerusalem) kutoka Tel Aviv.
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amewaambia viongozi hao kuwa, kwa mujibu wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na sheria zote za kimataifa. Quds Mashariki ni mji mkuu wa nchi huru ya Palestina.
Msimamo huo umechukuliwa baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kumtaarifu Kiongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas kwamba anakusudia kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tele Aviv na kuupelekea Quds Tukufu (Jerusalem).
Hatua hiyo inapingana na maamuzi na maazimio ya Umoja wa Mataifa yanayoitambua Quds Mashariki kuwa ni mji mkuu wa Palestina.
Katika kampeni zake za uchaguzi wa rais wa mwaka jana nchini Marekani Trump aliahidi kuwa ataitambua rasmi Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala ghasibu wa Israel na kuhamishia huko ubalozi wa Marekani.