Silaha za Marekani na Israel zapatikana katika ngome za ISIS, Syria
Siku chache baada ya Mkuu wa Jeshi la Russia kutangaza kuwa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) limeangamizwa kikamilifu nchini Syria, shehena ya silaha zilizotengenezewa Marekani na Israel imepatikana na wanajeshi wa Syria katika mji wa Dayr al-Zawr, iliyokuwa ngome ya mwisho ya magaidi hao.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Syria SANA, silaha hizo zilizoachwa na Daesh baada ya kufurushwa mjini hapo ni pamoja na mabomu ya kutegwa ardhini, mada za miripuko, vifaa vya mawasiliano, vifaru vya kijeshi na silaha nyinginezo.
Kamanda wa Jeshi la Syria amenukuliwa na SANA akisema kuwa, kupatikana silaha hizo zilizoundwa Marekani na Israel katika maficho ya Daesh ni ithibati tosha kuwa Tel Aviv na Washington ndizo zinazochochea machafuko na ukosefu wa uthabiti katika eneo kwa maslahi yao.
Jeshi la Syria lilifanikiwa hivi karibuni kuangamiza pote la mwisho la kundi la kigaidi la ISIS katika mji wa Dayr al-Zawr mashariki mwa Syria.
Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kwa mashambulio makali yaliyofanywa na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao kwa lengo la kubadilisha mlingano wa nguvu za kijeshi katika Mashariki ya Kati kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Kufuatia hatua hiyo Syria iliziomba Iran na Russia ziisaidie katika vita vya kupambana na magaidi hao.