Watawala vibaraka wa Kiarabu wabanwa; wananchi wataka viongozi wapya
Malalamiko na maandamano ya wananchi wa nchi za Kiarabu si tu kwamba yamewalenga Rais Donald Trump wa Marekani na Benjamin Netanyahi, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel pekee bali pia watawala vibaraka wa Kiarabu wanafanya eti mapatano ya amani na Wazayuni kwa madhara ya ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.
Ukweli wa mambo ni kuwa hatua ya Trump kutangaza mji Mtakatifu wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa israel na kisha kuamuru ubalozi wa nchi hiyo ulioko mjini Tel Aviv kuhamishiwa katika mji huo imedhihirisha wazi pengo kubwa lililoko katika ulimwengu wa Kiarabu. Kuna pengo kubwa lililoko baina ya utambulisho na matakwa ya raia wa nchi za Kiarabu na utambulisho wa kisiasa wa watawala wao ambao kimsingi ni vibaraka wanaohudumia maslahi ya nchi za Magharibi. Jambo hilo linathibitisha wazi kwamba watawala hao hawahudumii matakwa ya wananchi wala kuungwa mkono nao. Katika hali ambayo wananchi katika nchi nyingi za Kiarabu wamechukua msimamo mmoja wa kulaani vikali hatua hiyo ya Trump, tawala nyingi za Kiarabu zinazofanya mapatano na maadui wa Uislamu na hasa Saudi Arabia zimeamua kukaa kimya na hivyo kuamsha hasira ya wananchi na hata baadhi ya wanansiasa wa nchi hizo kulaani kimya hicho cha watawala wa Kiarabu.
Kwa kuzingatia suala hilo wananchi wa Jordan wamefanya maandamano ya kuunga mkono Quds Tukufu na wakati huohuo kupiga nara za kuwalaani Trump. Netanyahu na Muhammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia. Radiamali dhaifu na hata inayounga mkono hatua ya hivi karibuni ya Trump, iliyoonyeshwa na baadhi ya nchi za Kiarabu na hasa Saudi Arabia, jambo lililodhihiri wazi katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Kiarabu huko Cairo Misri, imekosolewa vikali na mawawziri wenzao katika nchi nyingine, Ibrahim al-Jaafari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema kwamba msimamo uliochukuliwa na mawaziri hao wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ni dhaifu sana na na usioendana na tishio linalohatarisha Quds Tukufu kwa sasa.
Lebanon pia imesema kuwa taarifa iliyotolewa mwishoni mwa kikao cha Cairo haiendani na uzito wa tishio linalohatarisha mustakbali wa Palestina. Ukweli ni kuwa hata kabla ya Marekani kutangaza rasmi kuutambua mji mtukufu wa Quds kuwa mji mkuu mpya wa utawala ghasibu wa Israel,tayari ilikuwa inafahamu vyema kwamba watawala vibaraka wa Kiarabu na hasa wale wanaodai kuongoza ulimwengu wa Kiaranu, wanapinga hatua hiyo kwa maneno tu na kuw ahawawezi kufanya lolote kuipinga, bali wanaridhishwa nayo. Katika hali ambayo, wananchi wa Palestina tayari wameanzisha Intifadha ya nne na kuungwa mkono na raia wa nchi zote za Kiarabu na hata mawakili wa Jordan kutangaza kuwa watawashtaki Trump na Netanyahu katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai iliyo na makao makuu yake mjini The Hague nchini Uholanzi, watawala vibaraka wa Kiarabu wanajishughulisha kuandaa vikao visivyo na maana wala natija yoyote, ambavyo mwishowe vinatoa taarifa dhaifu na zisizoweza kutekelezwa.
Mfano wa vikao hivyo ni kile ambacho kinafanyika leo mjini Cairo kikiwashirikisha Rais Abdulfattah as-Sisi wa Misri, Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Mfalme Abdallah wa Pili wa Jordan.
Kwa kutilia maanani hali hiyo na katika kuakisi maandamano ya watu wa Mashariki ya Kati dhidi ya hatua ya upande mmoja ya Trump kuutangaza mji wa Quds kuwa mji mkuu mpya wa utawala haramu wa Isreal, televisheni ya Marekani ya CNN ilesema kuwa wananchi wa eneo sasa wanataka kutawaliwa na viongozi wapya na kuchukuliwa misimamo mipya katika nchi za Kiarabu.