UN yaitaka Saudia iache kuwakandamiza watetezi wa haki za binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i38449-un_yaitaka_saudia_iache_kuwakandamiza_watetezi_wa_haki_za_binadamu
Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameitaka Saudi Arabia ikomeshe ukandamizaji wa watetezi wa haki za binadamu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 03, 2018 00:31 UTC
  • UN yaitaka Saudia iache kuwakandamiza watetezi wa haki za binadamu

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameitaka Saudi Arabia ikomeshe ukandamizaji wa watetezi wa haki za binadamu nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na wataalamu hao jana Jumanne, imeutaka utawala wa Aal-Saud uwaachie huru makumi ya watu uliowakamata tangu mwezi Septemba mwaka uliomalizika hadi sasa, kwa kutekeleza haki yao ya msingi na ya kijamii ya kuandamana.

Watalaamu hao wa haki za binadamu wa UN wamesema: "Tunashuhudia unyanyasaji mkubwa na ulioratibiwa dhidi ya watetezi wa haki za binadamu kwa kutekeleza haki yao ya kisiasa, uhuru wa kujumuika na kujieleza."

Maafisa wa polisi Saudia

Wameeleza wasi wasi wao kutokana na mwenendo wa kutisha wa kukamatwa na kuwekwa kizuizini shakhsia wa kidini, waandishi, waandishi wa habari, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu nchini humo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Kwa mujibu wa takwimu na ripoti za ndani nchini Saudia, zaidi ya wanaharakati wa kisiasa na wanasheria elfu 30 wanashikiliwa katika jela mbalimbali za utawala huo wa Aal-Saud.