Misri yatoa sharti kwa Hamas la kufanikisha maridhiano ya Wapalestina
Gazeti la Ra'yul-Yaum linalochapishwa London, Uingereza limeripoti kuwa serikali ya Misri imetoa masharti kwa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS ili kutekeleza maombi ya harakati hiyo.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, vyombo vya Intelijinsia vya Misri vimeijulisha HAMAS kuwa ikiwa harakati hiyo inataka yapatikane mafanikio katika suala la kufunguliwa vivuko vya kuingilia Ukanda wa Gaza, kukamilishwa mardhiano ya kitaifa na harakati ya Fat-h na vilevile kukamilishwa mapatano kati ya Hamas na serikali ya Cairo, lazima serikali hiyo iwe ndio kiunganishi na msuluhishi pekee wa kukamilisha kupatikana maridhiano ya kudumu na ya msingi.
Gazeti la Ra'yul-Yaum limemnukuu afisa mmoja wa serikali ya Misri akisema kuwa yapata wiki mbili nyuma, Naibu Mkuu wa vyombo vya Intelijinsia vya nchi hiyo aliwaeleza wawakilishi wa Hamas kuwa Misri haitaki Qatar na Uturuki ziiingilie suala la maridhiano na mapatano ya ndani baina ya Wapalestina, bali inataka Cairo pekee ibebe jukumu la kusimamia mazungumzo ya kutafuta maridhiano hayo.
Na hii ni katika hali ambayo ujumbe wa Harakati ya Hamas leo umeelekea Misri ili kukamilisha mazungumzo na maafisa wa usalama na Intelijinsia wa nchi hiyo.
Sambamba na hayo ujumbe wa harakati ya Fat-h jana uliwasili mji mkuu wa Qatar, Doha kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Hamas kuhusiana na maridhiano ya ndani ya Wapalestina.../