Maulamaa wa Pakistan watoa fatua ya kuharamisha kujiripua
Mamia ya maulamaa wa Kiislamu nchini Pakistan wametoa fatua ya kuharamisha mashambulizi ya kujitoa muhanga, katika hali ambayo nchi hiyo inaendelea kukabiliwa na hujuma za magenge ya kigaidi.
Katika kitabu kilichozinduliwa na serikali jana Jumanne mjini Islamabad, wanazuoni 1,800 wa Pakistan kwa kauli moja wamepasisha kuwa 'mashambulizi ya kujitoa muhanga ni haramu'.
Wasomi hao wa Kiislamu ambao wametangaza kuwa hakuna mtu au kundi lolote lenye mamlaka ya kutangaza eti vita vitakatifu, wamesema mashambulizi ya bomu ya kujitoa muhanga yanaenda kinyume na mafundisho ya Kiislamu.
Akihutubu katika hafla ya kuzinduliwa kitabu hicho, Rais Mamnoon Hussain amesema ana imani kuwa fatua hiyo ya pamoja ya wanazuoni wa nchi hiyo itatoa mchango mkubwa katika vita dhidi ya ugaidi, misimamo ya kuchupa mipaka na chuki za kimadhehebu.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Ahsan Iqbal, amesema ni jambo la kutia hofu kwamba baada ya miaka 70, ndoto za Wapakistani za kuona taifa lao ni la heshima na lenye kufuata mfumo wa haki hazijatimia mpaka sasa.
Maelfu ya wananchi wa Pakistan wamepoteza maisha katika mashambulizi ya mabomu na hujuma nyingine za kigaidi tangu mwaka 2001, wakati nchi hiyo iliporubuniwa na Washington na kuingia katika muungano wa kijeshi wa Marekani eti wa kupambana na ugaidi.