Mshindi wa Nobel asema Saudia na Imarati zimeisaliti Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i40093-mshindi_wa_nobel_asema_saudia_na_imarati_zimeisaliti_yemen
Tawakkol Karman, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel wa nchini Yemen amesema Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zimeisaliti nchi yake kwa kuivamia kijeshi na kuifanya ishuhudie moja ya migogoro mikubwa zaidi duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 08, 2018 10:46 UTC
  • Mshindi wa Nobel asema Saudia na Imarati zimeisaliti Yemen

Tawakkol Karman, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel wa nchini Yemen amesema Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zimeisaliti nchi yake kwa kuivamia kijeshi na kuifanya ishuhudie moja ya migogoro mikubwa zaidi duniani.

Katika mahojiano kwa njia ya simu na shirika la habari la Reuters akiwa mjini Istanbul nchini Uturuki, mwanaharakati huyo amesema ni jambo la kusikitishwa namna Saudia na Imarati zimeamua kukandamiza mabadiliko ya kidemokrasia nchini Yemen, kurejesha nyuma saa ya maendeleo ya kisiasa katika nchi hiyo jirani yake na kuzima vuguvugu la 'Machipuo ya Nchi za Kiarabu', yote hayo kwa shabaha ya kupanua satua na kuimarisha ushawishi wake katika eneo.

Amesisitiza kuwa, "Mustakabali wa Machipuo ya Kiarabu ni mustakabali wa mabadiliko, na katu gurudumu la historia haliwezi kurudi nyuma."  

Tawakkol Karman, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel 

Mapema mwezi huu, mshindi huyo wa tuzo ya kifahari ya Nobel mwaka 2011 alisema kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa, kwa sasa anakusudia kuwashirikisha wanaharakati wote wa haki za binaadamu katika kuwasilisha mashitaka yao katika mahakama za kimataifa dhidi ya Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme nchini Saudia na Mohammed bin Zayed Al Nahyan, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Abu Dhabi kutokana na jinai zao za mauaji ya umati nchini Yemen.

Hivi karibuni, maelfu ya wanawake wa Yemen waliandamana katika mji mkuu Sana'a wakilalamikia na kulaani mashambulio ya muungano vamizi wa kijeshi wa Saudi Arabia dhidi ya nchi yao, ambayo yameendelea kuua maelfu ya raia wasio na hatia yoyote, tangu Machi mwaka 2015.