Mansour Hadi avunja ukimya; aituhumu Imarati kwa kuvuruga uthabiti Yemen
Rais wa zamani wa Yemen Abdu Rabbuh Mansour Hadi hatimaye amevunja kimya chake na kuituhumu Imarati kuwa inadhoofisha na kuvuruga hali ya uthabiti huko Yemen.
Hadi ambaye imeelezwa kuwa yuko chini ya kifungo cha nyumbani nchini Saudia ametoa mkanda wa sauti uliorekodiwa kutoka Riyadh akisema kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) umehusika katika machafuko ya karibuni katika mji wa Aden huko Yemen. Rais huyo mtoro wa Yemen ameongeza kuwa Imarati inapanga mapinduzi katika mji huo wa bandari wa kusini mwa Yemen.
Ameendelea kubainisha kuwa utawala wa Imarati unafuatilia maslahi yake binafsi huko Yemen huku ukishindana na Saudi Arabia ili kuwa na ushawishi katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu. Saudi Arabia ilianzisha ita vya umwagaji damu huko Yemen mapema mwaka 2015 ikiwa ni katika jitihada zake za kumrejesha madarakani kibaraka wake huyo Abdu Rabbuh Mansour Hadi ili kuwaangamiza wapiganaji wa Kihuthi wenye mamlaka ya uongozi katika mji mkuu Sana'a.