Hujuma za anga za Marekani zaendelea kuteketeza roho za Wasyria
Makumi ya raia wameuawa kufuatia mashambulizi ya anga ya Marekani mashariki mwa mkoa wa Dayr al-Zawr nchini Syria.
Shirika rasmi la habari la serikali nchini Syria SANA limetangaza kuwa, hujuma hizo za ndege za kijeshi za Marekani zimelenga kambi ya wakimbizi wa ndani katika mji wa Dhahret al-Allouni, mashariki mwa Dayr al-Zawr na kuua raia 24 jana Jumanne.
Habari zaidi zinasema mashambulizi hayo ya anga ya Marekani kadhalika yamejeruhi idadi kubwa ya watu mbali na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu katika eneo hilo.
Hujuma hizo zimefanyika masaa machache baada ya Damascus kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiagiza Marekani isitishe eti operesheni dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) katika hali ambayo inaua raia wasio na hatia wa Syria.
Siku tatu zilizopita, Marekani iliua raia wengine 29 na kujeruhi makumi ya wengine katika hujuma nyingine za anga katika vijiji vya al-Sha'afa na Dharat Allouni mkoani Dayr al-Zawr.
Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 wakati magaidi walipoivamia nchini hiyo kwa himaya ya Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao wakiwemo Uingereza na Ufaransa kwa lengo la kubadilisha mlingano wa kieneo kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kufuatia hujuma hiyo, Syria iliomba msaada wa Russia na Iran katika kuisaidia kukabiliana na magaidi.