Wapalestina wasusia mkutano wa White House, Israel na Waarabu kuhusu Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i41653-wapalestina_wasusia_mkutano_wa_white_house_israel_na_waarabu_kuhusu_gaza
Mamlaka ya Ndani ya Palestina imekataa kushiriki mkutano uliofanyika katika Ikulu ya Marekani ya White House, na kuwaleta pamoja viongozi wa nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 14, 2018 10:47 UTC
  • Wapalestina wasusia mkutano wa White House, Israel na Waarabu kuhusu Gaza

Mamlaka ya Ndani ya Palestina imekataa kushiriki mkutano uliofanyika katika Ikulu ya Marekani ya White House, na kuwaleta pamoja viongozi wa nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mkutano huo wa jana Jumanne uliojadili hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza ulihudhuriwa na utawala haramu wa Israel, nchi 17 zikiwemo Saudi Arabia, Canada na nchi kadhaa za Ulaya.

Jason Greenblatt, mwakilishi maalumu wa Donald Trump katika mgogoro wa Palestina na Israel amesema, "Tunasikitika kwamba Mamlaka ya Ndani ya Palestina haipo nasi kwenye mkutano huu hii leo." Aidha amedai kuwa Harakati ya Mapambano ya Palestina Hamas, ndiyo inabeba dhima ya matatizo yote yanayowakabili Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Vifaru vya Wazayuni katika Ukanda wa Gaza

Hii ni katika hali ambayo, kuanzia mwaka 2007 utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha mzingiro wake dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na kuzuia kuingizwa katika eneo hilo vifaa na huduma muhimu kama dawa, mafuta na bidhaa za kimsingi. 

Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeususia mkutano wa White House uliohudhuriwa pia na Jared Kushner, mume wa binti ya Trump; kulalamikia hatua ya Washington mwezi Disemba mwaka jana, ya kuitangaza Quds Tukufu (Jerusalem) kuwa eti mji mkuu wa utawala haramu wa Israel na kusema kuwa Marekani itauhamishia ubalozi wake mjini hapo kutoka Tel Aviv.