Malengo ya safari ya Bin Salman nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i41964-malengo_ya_safari_ya_bin_salman_nchini_marekani
Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman jana Jumanne aliwasili Washington nchini Marekani kwa ziara ya wiki mbili.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Mar 21, 2018 03:39 UTC
  • Malengo ya safari ya Bin Salman nchini Marekani

Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman jana Jumanne aliwasili Washington nchini Marekani kwa ziara ya wiki mbili.

Safari hiyo ya Bin Salman nchini Marekani inafanyika baada ya kuzitembelea nchi za Misri na Uingereza.

Katika safari yake ya sasa nchini Marekani, Bin Salman anafuatilia malengo kadhaa. Mtandao wa habari wa The Atlantic Council umeandika kuwa: "Inatazamiwa kuwa, ajenda kuu ya Bin Salman katika safari yake nchini Marekani itaakisi siasa na sera zake pana za kupenda makuu na jaha. Kuna uwezekano mkubwa kwamba atajadili masuala ya jiografia ya kisiasa, usalama wa nishati na uwekezaji. Vilevile atazungumzia marekebisho ya kijamii na kiuchumi yaliyoanzishwa na utawala wa kifalme wa Saudi Arabia", mwisho wa kunukuu.

Bin Salman

Hii ni mara ya kwanza kwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia kutembelea Marekani tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo katika kile kinachoaminika kuwa ni mapinduzi baridi. Muhammad bin Salman aliteuliwa kuwa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia Juni mwaka jana baada ya safari ya Donald Trump huko Saudia ambako aliona kwa macho jinsi kijana huyo alivyotumia fedha nyingi kwa ajili ya mapokezi ya Rais wa Marekani. Sasa kijana huyo anafanya ziara nchini Marekani akisubiri kutangazwa rasmi kama Mfalme wa Saudia. Bin Salman mwenyewe ameiambia televisheni ya CBS ya Marekani kwamba, kifo pekee ndicho kinachoweza kumzuia kuwa mfalme wa Saudi Arabia. Katika safari hii Bin Salman anafanya jitihada za kuhakikisha kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya ufalme wa Saudia anamshawishi Donald Trump ili mfalme mpya wa Saudi Arabia atangazwe wakati wa uhai wa mfalme wa sasa wa nchi hiyo ili asije akakumbana na misukosuko na matatizo ya ugomvi wa kuwania madarakani na ndugu zake baada ya kuaga dunia Mfalme Salman. 

Trump na Bin Salman, Washington

Hapana shaka pia kwamba moja kati ya ajenda kuu za safari ya Bin Salman nchini Marekani ni masuala ya jiografia ya kisiasa na kuimarisha kambi dhidi ya Iran. Katika suala hilo Trump na baadhi ya mawaziri wenye misimamo mikali katika serikali yake kama Waziri mpya wa Mashauri ya Kigeni, Mike Pompeo wako bega kwa bega na Bin Salman. Muhammad bin Salman anaamini kuwa, Iran si mpinzani wa Saudi Arabia bali ni adui wake na ameamua hata kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel, adui mkubwa wa Umma wa Kiislamu na nchi za Kiarabu, kwa ajili tu ya kufikia malengo yake ya kihasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Bin Salman ambaye amezama katika kinamasi cha Yemen, amepigwa konde la nguvu huko Syria, na nchini Lebanon ameshindwa kufikia malengo yake dhidi ya harakati ya Hizbullah. Kijana huyu mwanagenzi anaamini kwamba, Saudia imepigwa makonde hayo yote katika eneo la Mashariki ya Kati kutokana stratijia za Iran. Kwa msingi huo katika safari yake ya sasa mjini Washington, Bin Salman atafanya jitihada za kuhakikisha anatoa kitita kikubwa cha pesa katika kalibu ya manunuzi ya silaha mpya na kuishawishi Marekani izidishe mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni pamoja na kuiwekea vikwazo katika suala la utengenezaji wa makombora ya masafa marefu au hata Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Hayo yanafanyika sambamba na kuvuja habari kwamba, Imarati, mwitifaki wa karibu wa Saudia, ilikuwa na ushawishi ndani ya White House katika kufutwa kazi aliyekuwa waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson.

Mfalme wa Saudia akimvisha Trump nishati ya Abdulaziz al-Saud 

Masuala mengine yanayotarajiwa kujadiliwa katika mazungumzo ya Bin Salman na maafisa wa Marekani ni mvutano uliopo baina ya Saudia na Qatar, vita vya Yemen na chaguzi za Iraq na Lebanon. James Reinl ameandika katika mtandao wa The Middle East Eye kwamba: "Mvutano uliopo baina ya Saudia na Qatar ni muhimu zaidi kwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia kuliko maudhui nyingine kwa sababu nchi ndogo ya Qatar imeweza kutoa changamoto kwa Saudia inayodai kuwa kinara wa nchi za Kiarabu. Kwa hakika mapambano ya Qatar na kusimama kwake kidete dhidi ya mashinikizo ya Saudia yamelenga uongozi wa Saudi Arabia katika ulimwengu wa Kiarabu na kwa msingi huo Bin Salman atafanya jitihada kuhakikisha kwamba, White House inazidisha mashinikizo dhidi ya serikali ya Doha", mwisho wa kunukuu.

Image Caption

Lengo jingine linalofuatiliwa na Muhammad bin Salman katika safari yake ya sasa nchini Marekani ni kujaribu kuishawishi Kongresi ya nchi hiyo ifute sheria ya Jasta. Sheria hiyo inayojulikana kama The Justice Against Sponsors of Terrorism Act, (JASTA) kwa kifupi, ilipasishwa katika Kongresi ya Marekani Septemba mwaka 2016 na kuziruhusu familia za wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani kufungua mashtaka dhidi ya Saudi Arabia na kudai fidia. Kuhusu suala hilo gazeti la al Masriyyun limeandika kuwa: "Kanuni ya Jasta ni sawa na "hanjari katika mgongo wa Saudi Arabia". Hata wakati wa safari ya Donald Trump nchini Saudia mwaka jana, Riyadh ilifanya jitihada kubwa za kumshawishi Rais huyo wa Marekani afanye juhudi za kufuta sheria hiyo. Trump anatambuliwa kuwa muungaji mkono mkubwa wa Jasta.