Kuendelea kujitanua Israel katika kivuli cha uungaji mkono wa Marekani
Vyombo vya habari vimetangaza juhudi zinazofanywa na utawala haramu wa Israel kwa ajili ya kujenga maelfu ya nyumba mpya katika ardhi za Wapelestina.
Ikiwa ni katika kuendeleza siasa zake za kujitanua katika ardhi hizo, baraza la mawaziri la Benjamini Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo wa kizayuni siku ya Alkhamisi lilipitisha mpango wa kujengwa nyumba nyingine 4000 katika maeneo tofauti ya ardhi unazizokalia kwa mabavu za Palestina. Duru hii mpya ya ujenzi wa nyumba hizo ambazo zinalenga kuwapa makazi Wazayuni zaidi na vilevile kueneza vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina inayokaliwa kwa mabavu, kwa hakika ni jambo ambalo linaenda sambamba na uchochezi wa viongozi wa Marekani kwa ajili ya kutoa mwanya kwa utawala huo kujitanua zaidi katika ardhi hizo. Kuhusiana na suala hilo, David Friedman, Balozi wa Marekani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina amesema kuwa ujenzi wa vitongoji vya Wazayuni katika ardhi hizo ni wa kisheria.
Hatua ya Rais Doland Trump wa Marekani ya kumteau Friedman, ambaye ana misimamo ya kupindukia na upendeleo wa moja kwa moja kwa utawala wa Kizayuni, kuwa balozi wa nchi hiyo huko Israel kwa hakika inabainisha wazi ishara ya Washington kwa utawala huo uendelee kudumisha siasa zake za kujitanua katika ardhi za Wapalestina. David Friedman ambaye alikuwa wakili na mshauri maalumu wa Trump katika kampeni zake za uchaguzi, ni mmoja wa waungaji mkono wakubwa wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na Kiyahudi katika ardhi zilizoghusubiwa za Wapalestina na pia mtetezi mkuu wa siasa za rais huyo wa Marekani za kuutambua mji mtukufu wa Quds kuwa eti ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, na hatimaye kuhamishiwa ubalozi wa Marekani katika mji huo ambao ni Kibla cha kwanza cha Waislamu.
Mwishoni mwa mwaka uliopita, Trump alichukua uamuzi wa kichochezi wa kuutambua mji wa Quds Tukufu kuwa eti mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, na tokea wakati huo utawala wa Kizayuni umekuwa ukitumia vibaya fursa hiyo kujitanua zaidi katika ardhi za Wapalestina na hasa katika mji wa Quds Tukufu.
Kwa kujaribu kubadilisha ramani ya kijografia ya maeneo ya Palestina, utawala haramu wa Israel unafanya kila unaloweza kujizatiti zaidi katika maeneo hayo. Hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa na ya Geneva, utawala wa Israel ambao unahesabiwa kuwa ni utawala vamizi na unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina hauna ruhusa ya kubadili muundo wa kijamii au wa kijografia wa ardhi hizo. Kuhusian ana suala hilo, Hannan Ashrawi, mjumbe wa kamati andamizi ya Chama cha ukombozi wa Palestina PLO ameutuhumu utawala huo haramu kuwa unafanya juhudi kubwa za kubadili maeneo ya Wapalestina ukiwemo mji wa Quds, kuwa ya Wazayuni na kusisitiza kuwa ni serikali ya Marekani ndiyo imewachochea watawala wa Israel kuchukua hatua hiyo ya kidhalimu. Amesisitiza kuwa kama usingekuwa ni uungaji mkono wa serikali ya Trump, Israel isingethubutu kuchukua hatua kama hiyo. Ukweli wa mambo ni kwamba ushirikiano wa watawala wa Israel na Marekani umepata msukumo mpya kufuatia kuingia madarakani Trump, ambapo sasa ushirikiano wa pande mbili hauishii tu katika msaada wa kila mwaka wa kifedha na kijeshi wa Marekani kwa utawala huo.
Mapatano ya pande mbili ya kubuni kamati ya pamoja na kushughulikia masuala ya ujenzi wa vitongoji ambayo yalitangazwa na Benjamin Netanyahu mara tu baada ya kureja Israel kutoka Marekani ni suala linalopasa kuzingatiwa kwa makini katika uwanja huo. Ushirikiano wa Netanyahu na Trump katika kueneza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, suala ambalo kwa hakika ni kikwazo kikuu katika kubuniwa nchi huru ya Palestina, mji mkuu wake ukiwa ni Quds Tukufu, ni suala linalothibitisha wazi kwamba kila mpango anaopangwa na Netanyahu unatekelezwa kivitendo na Trump, jambo linaloonyesha wazi kwamba Marekani hivi sasa inashiriki kwa nguvu zake zote katika siasa za kujitanua utawala haramu wa Israel katika ardhi za Palestina, kuliko wakati mwingine wowote.