Hamas yakana kuzungumza na Misri kuhusu askari mateka wa Israel
Afisa mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amekanusha madai ya kuwepo aina yoyote ya mazungumzo baina ya harakati hiyo na Misri kuhusu askari wa Israel wanaoshikiliwa mateka na Hamas.
Mahmoud al Zahhar amesema kuwa hadi sasa hakujafanyika mazungumzo ya aina yoyote baina ya tawi la kijeshi la Hamas, Brigedia ya Izzuddin Qassam na maafisa wa serikali ya Misri kuhusu askari mateka wa Israel.
Kuhusu tuhuma dhidi ya Hamas kwamba inahusika katika machafuko na mapigano ya sasa nchini Misri, al Zahhar amesema kuwa, Hamas kamwe haijahusika katika machafuko hayo.
Afisa huyo mwanadamizi wa Hamas amesema ameshiriki katika mazungumzo ya Cairo kuhusu kivuko cha Rafah huko kusini mwa Gaza na kwamba Hamas imewataka Wamisri wafungue daima kivuko hicho cha mpakani kwa sababu suala hilo lina umuhimu mkubwa kwa raia wa Palestina wanaozingirwa kila upande na utawala haramu wa Israe kwa miaka kadhaa sasa.