Daesh watumia silaha za kemikali dhidi ya uwanja wa ndege Syria
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limeshambulia uwanja wa ndege wa kijeshi mashariki mwa Syia, kwa silaha za kemikali.
Kanali ya televisheni ya Ikhbariyah ya Syria imeripoti kuwa, Jumatatu jioni magaidi hao wa kitakfiri walivurumisha maroketi yaliyokuwa na kemikali ya sumu aina ya haradali (mustard) katika uwanja wa ndege wa kijeshi kusini mwa mji wa Dayr al-Zawr, mashariki mwa nchi.
Hata hivyo haikubainika mara moja iwapo kulikuwa na maafa au manusura katika hujuma hiyo ya jana.
Haya yanajiri katika hali ambayo, mwezi Febuari mwaka huu, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA lilisema kuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh linatumia silaha za kemikali katika mashambulizi yake.
Mbali na Syria, kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh linatumia silaha hizo za kemikali katika mashambulizi yake nchini Iraq.
Siku chache zilizopita, jeshi la Iraq kwa kushirikiana na harakati za wananchi lilifanikiwa kumuua kiongozi wa kundi hilo la kigaidi anayefahamika kama Abbas al-Kurdi, aliyehusika katika ufyatuaji wa silaha za kemikali mjini Kirkuk nchini Iraq.