Wapalestina 3 waaga dunia kutokana na majeraha ya risasi za Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i44730-wapalestina_3_waaga_dunia_kutokana_na_majeraha_ya_risasi_za_israel
Wapalestina watatu waliojeruhiwa vibaya na risasi za jeshi katili la Israel katika Ukanda wa Gaza wiki iliyopita wamefariki dunia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 19, 2018 23:34 UTC
  • Wapalestina 3 waaga dunia kutokana na majeraha ya risasi za Israel

Wapalestina watatu waliojeruhiwa vibaya na risasi za jeshi katili la Israel katika Ukanda wa Gaza wiki iliyopita wamefariki dunia.

Wizara ya Afya ya Gaza imewataja mashahidi hao ambao wameaga dunia kutokana na majeraha mabaya waliyosababishiwa na risasi za Israel kama Moein al-Saai, aliyekuwa na umri wa miaka 58, Mohammed Mazen al-Ayyan, miaka 20 na Ahmad Abu Samareh, aliyekuwa na miaka 21.

Vifo hivyo vimepelekea idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi katika maandamano ya amani ya Jumatatu iliyopita katika Ukanda wa Gaza kukaribia 70.

Takwimu zinaonyesha kuwa, Wapalestina 106 wameuawa shahidi na askari wa utawala vamizi wa Israel, wakiwemo watoto 15 tangu maandamano ya Wapalestina ya "Haki ya Kurejea" yalipoanza tarehe 30 Machi.

Mashahidi 3 wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza

Wapalestina wengine zaidi ya 12,000 wamejeruhiwa katika kipindi hicho, huku Wapalestina 3,500 miongoni mwao wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi za moto na askari wa Kizayuni.

Hii ni katika hali ambayo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya utawala haramu wa Israel imepinga vikali uamuzi wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa wa kutaka wachunguzi wa kimataifa wa jinai za vita wapelekwe haraka Ukanda wa Gaza, Palestina inayokaliwa kwa mabavu kufanya uchunguzi kuhusu mauaji ya kinyama ya Wapalestina yaliyofanywa na askari wa Israel.