Associated Press: Imarati imetengeneza "Abu Ghuraib" huko Aden
Shirika la habari la Associated Press limefichua kashfa mpya ya makamanda wa jeshi la Imarati na mawakili wao dhidi ya mamia ya Wayemen wanaoshikiliwa katika jela ya mji wa Aden huko kusini mwa Yemen.
Shirika hilo limefananisha mbinu za mateso zinazotumiwa na makamanda wa jeshi la Yemen na vibaraka wao kuwatesa raia hao wa Yemen na zile zilizokuwa zikitumiwa na askari wa Marekani katika jela ya kutisha ya Abu Ghuraib nchini Iraq.
Ripoti ya Associated Press inasema Imarati ina jela zisizopungua tano za siri katika eneo la Aden ambazo mbinu zake za mateso zinashabihiana na hata kuzidi zile zilizokuwa zikitumiwa na Wamarekani katika jela ya kutisha ya Abu Ghuraib nchini Iraq.
Associated Press imefichua badhi ya mateso na ukatili unaofanywa na askari wa Umoja wa Falme za Kiarabu dhidi ya Wayemen wanaoshikiliwa katika jela hizo ukiwemo udhalilishaji na ukatili wa kingono.
Baadhi ya mateka wa Yemen wanaoshikiliwa katika jela ya Biir Ahmad wamevuliwa uchi wa mnama, kulawitiwa na kuteswa maeneo yao ya siri kwa kutumia nyaya za umeme.
Ripoti ya Associated Press inasema: Baadhi ya Wayemen walioteswa kwa kulawitiwa katika jela hizo wamesema kwamba, walitamani kufariki dunia badala ya kukumbana na mateso na udhalilishaji huo mkubwa. Baadhi yao pia wamesema kuwa makamanda wa jeshi la Imarati wanashirikiana na askari wanaosadikiwa kuwa ni Wamarekani na wengine kutoka nchi za America ya Latini.