Lavrov: Matatizo ya Mashariki ya Kati yatatatuliwa kwa kuishirikisha Iran
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia amesisitiza kuwa, kuitaka Iran ipunguze ushawishi wake nchini Syria na Mashariki ya Kati ni kutazama mambo bila ya kuzingatia uhalisia wake.
Sergei Lavrov amesema hayo mjini Moscow katika mkutano wake wa pamoja na waandishi wa habari akiwa na mgeni wake Ayman Safadi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jordan na kusema bayana kwamba, matatizo ya Mashariki ya Kati hayawezi kupatiwa ufumbuzi pasina ya kuzishirikisha nchi muhimu za eneo hili ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia kadhalika amesema kuwa, vikwazo vyote dhidi ya Syria vinapaswa kuondolewa sambamba na kuchukuliwa hatua zinazofaa kwa ajili ya kudhamini usalama wa kurejea wakimbizi wa nchi hiyo.
Sergei Lavrov amekumbusha nafasi ya Jordan ikiwa msimamizi wa mazungumzo ya Astana ambayo duru yake ijayo itafanyika mwishoni mwa mwezi huu na kusema kuwa, nafasi ya Amman katika uwanja huo ni muhimu na yenye thamani mno.
Aidha amezungumzia mzozo wa utawala haramu wa Israel na Palestina na kueleza kwamba, kuna haja ya kuchukuliwa hatua zaidi za pamoja kwa ajili ya kuleta amani na uthabiti katika Mashariki ya Kati.
Kwa upande wake Ayman Safadi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jordan amesisitiza juu ya amani na matakwa ya kimataifa na kusema kuwa, nchi yake inafungamana na suala la kupatikana amani ya kudumu katika Masharikki ya Kati na inathamini mno nafasi na mchango chanya wa Russia katika uwanja huo.