Amnesty International yaitaka Saudia iwaachie huru watetezi wa haki za binadamu
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka jamii ya kimataifa kuishinikiza zaidi Saudi Arabia ili ikomeshe ukandamizaji na iwaachie huru wapinzani na wanaharakati wa masuala ya kijamii. Wito huo umetolewa baada ya utawala wa kizazi cha Aal Saud kuzidisha mashinikizo dhidi ya wapinzani wa serikali ya kifalme ya nchi hiyo na wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu.
Amnesty International imesema kuwa, katika miezi ya hivi karibuni Saudi Arabia imetia nguvuni na kusweka jela idadi kubwa ya wahadhiri wa vyuo vikuu, washairi, walingania wa kidini na mashekhe, na wafanya biashara kwa tuhuma za kuhujumu usalama wa taifa. Taarifa ya Amnesty International imeongeza kuwa, hatua hiyo imezusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu.
Taarifa hiyo imetolewa katika kipindi cha sasa ambapo uhusiano wa Saudi Arabia na Canada umeingiwa na misukosuko baada ya serikali ya Ottawa kueleza wasiwasi wake kuhusu wimbi la kamatakamata ya wanaharakati wa haki za binadamu na masuala ya kijamii nchini Saudia.
Kutokana na kushadidi ukandamiza na kamatakamata dhidi ya wapinzani wa serikali na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu na masuala ya kijamii nchini Saudi Arabia katika miezi ya hivi karibuni, nchi na taasisi mbalimbali za kimataifa zimeikosoa vikali mienendo ya serikali ya Riyadh na kutoa wito wa kusitishwa ukandamizaji nchini humo. Siasa hizo za ukandamizaji nchini Saudi Arabia zinatekelezwa wakati Mrithi wa Kiti cha Ufalme Muhammad bin Salman ambaye kimsingi ndiye anayeongoza nchi hiyo kwa sasa, amekuwa akifanya marekebisho yanayohusiana na masuala ya haki za wanawake na uhuru wa kijamii kwa matakwa ya nchi za Magharibi na kwa malengo ya kisiasa. Miongoni mwa haki zilizotolewa kwa wanawake wa Saudi Arabia ni pamoja na kupewa haki ya kuendesha magari, haki ya kutoka nje na kusafiri peke yao, kuzidishwa ajira za wanawake katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii na kupewa uhuru wa kuwepo katika maeneo ya umma.
Haki hizo ambazo ni miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakidaiwa na wanawake wa Saudi Arabia kwa miaka mingi, zimetolewa kidhahiri na kimaonyesho tu huku utawala wa kifalme wa nchi hiyo ukizidisha ukandamizaji dhidi ya wanaharakati wa haki za binadamu na wanawake wanaofanya kazi katika uwanja huo.
Sarah Leah Whitson ambaye ni Mkurugenzi wa Human Rights Watch kanda ya Mashariki ya Kati anasema: "Maafisa wa serikali ya Saudia chini ya usimamizi wa Bin Salman wamezidisha vitendo vya kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wanaharakati nchini humo na wanautambua upinzani wa aina yoyote kuwa ni tishio dhidi ya serikali yao ya kidikteta."
Idadi ya wafungwa wa kisiasa imefikia elfu thalathini nchini Saudi Arabia na vitendo vya kukamatwa na kuhumumiwa mahakamani kinyume cha sharia vinaongezeka siku baada ya siku nchini humo. Ukatili na ukandamizaji wa wanaharakati wa masuala ya kijamii nchini Saudi Arabia umekuwa mkubwa na kuvuka mipaka kiasi kwamba hata waitifaki wa Kimagharibi wa utawala huo hawawezi tena kunyamazia kimya uhalifu na ukiukaji huo mkubwa wa haki za binadamu. Kuhusu kadhia hiyo, mwakilishi wa Uingereza katika Bunge la Ulaya, Charles Tannock anasema: "Iwapo Saudia inataka kulinda nafasi yake katika eneo la Mashariki ya kati inapaswa kuhakikisha kwamba mfumo unaotawala sasa nchi hiyo unaoana na sheria za kimataifa."
Wakati huo huo wanaharakati wa masuala ya kisheria na kijamii wa Saudi Arabia wanataka kufanyike marekebisho halisi na ya kweli nchini humo na si kutumia nara na kaulimbiu ya marekebisho kama wenzo wa kutimizia malengo ya kisiasa. Yahya Assiri ambaye ni mwanaharakati wa haki za binadamu wa Saudi Arabia anasema: "Kama kweli Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman anataka kuonesha sura nzuri kuhusu nchi yake basi analazimika kufanya marekebisho ya kweli ndani ya nchi na kukomesha kukandamizaji wa wapinzani na wanaharakati."