Netanyahu akiri kuwa uwepo wa Israel uko hatarini
Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel amesema uwepo wa utawala huo uko hatarini.
Benjamin Netanyahu ameyasema hayo kufuatia maandamano yaliyofanyika mjini Tel Aviv kupinga sheria ya "Dola la Mayahudi Pekee".
Huku akiashiria kwamba katika maandamano ya kupinga sheria hiyo bendera za Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) zilipeperushwa katikati ya Tel Aviv, Netanyahu amesema: uwepo wa Israel unakabiliwa na hatari.
Maelfu ya wakaazi wa ardhi za Palestina zilizovamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948 na kupewa jina la Israel, Jumamosi usiku walifanya maandamano makubwa mjini Tel Aviv kupinga sheria ya "Dola la Mayahudi Pekee".
Maandamano hayo yalifanyika kuitikia wito wa kamati kuu ya kufuatilia masuala ya Waarabu wanaoishi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Washiriki wa maandamano hayo walibeba bendera za Palestina huku wakitoa miito ya shime na sha'ar za kutaka kufutwa sheria hiyo ya kibaguzi.
Bunge la utawala haramu wa Israel, Knesset, mnamo 19 Julai lilipitisha sheria ya 'Dola la Mayahudi Pekee'. Kwa mujibu wa sheria hiyo, ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo zinatambuliwa kuwa ni za Mayahudi pekee na kwamba Wapalestina wanaoishi katika ardhi hizo watanyimwa haki zote za kiraia na za kibinadamu.
Sheria hiyo ni sehemu ya mpango wa Marekani ujulikanao kama "Mapatano ya Karne" ulioandaliwa na serikali ya Washington na mchakato wa utekelezaji wake umeshaanza rasmi.../