Mitazamo ya Zarif kuhusu migogoro ya Mashariki ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i4744-mitazamo_ya_zarif_kuhusu_migogoro_ya_mashariki_ya_kati
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameliambia shirika la habari la Russia la Tass News Agency kwamba misimamo mikali na ugaidi vinatishia maeneo ya Mashariki ya Kati, Asia ya Kati na Kaukasia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 09, 2016 22:34 UTC
  • Mitazamo ya Zarif kuhusu migogoro ya Mashariki ya Kati

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameliambia shirika la habari la Russia la Tass News Agency kwamba misimamo mikali na ugaidi vinatishia maeneo ya Mashariki ya Kati, Asia ya Kati na Kaukasia.

Muhammad Javad Zarif amesema katika mahojiano hayo kwamba: Sisi sote tunakabiliwa na hatari ya misimamo mikali na ugaidi kwa msingi huo kuna udharura wa kutatua mivutano iliyopo kwa njia za amani kwa shabaha ya kuheshimu sheria za kimataifa na hati ya Umoja wa Mataifa.

Zarif amesema kuwa, ugaidi na misimamo mikali vinatokana na uvamizi na tabia ya baadhi ya tawala kukalia kwa mabavu ardhi za watu wengine na kuongeza kuwa, misimamo mikali na ugaidi ulishadidi zaidi baada ya miaka mingi ya kukaliwa kwa mabavu Iraq na hali iliyojitokeza baada yake.

Sambamba na kueleza mitazamo ya Iran katika uwanja wa kutatua migogoro ya Mashariki ya Kati, Dakta Muhammad Javad Zarif amekosoa vikali siasa za kindumakuwili za nchi zinazodai kuwa vinara wa kupambana na ugaidi. Amesema kuwa, jamii ya kimataifa hususan wale wanaosema maneno mengi kuhusu mapambano dhidi ya ugaidi na misimamo mikali wanawajibika kujifunza uwajibikaji, kuwa na azma imara na kuchukua hatua za kivitendo za kukabiliana na ugaidi badala ya kuchukua maamuzi matupu ya kisiasa. Amesisitiza kuwa inawezekana kutokomeza misimamo mikali na kusema kuwa, mapambano dhidi ya ugaidi na misimamo mikali yanahitajia mchakato wa pande kadhaa na kwamba mashambulizi ya kijeshi ni sehemu moja tu ya mapambano hayo.

Matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran yanaashiria siasa za kindumakuwili zinazotekelezwa na Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati. Hii ni kwa sababu sambamba na kutoa madai ya kupambana na ugaidi, Marekani imekuwa ikiyasaidia na kuyaunga mkono kwa siri makundi ya kigaidi na kuyatumia kwa ajili ya kutimiza malengo yake katika eneo hilo. La kusikitisha zaidi ni kuwa, katika safari yake ya Alkhamisi iliyopita huko Bahrain alikoshiriki kikao cha Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, alizitaja siasa za kuingia mambo ya nchi nyingine na kuzusha mifarakano za Washington kuwa zinaimarisha amani na usalama katika eneo la Mashariki ya Kati!

Katika safari hiyo mjini Manama, Kerry ambaye hakuashiria kabisa suala la kutokuwepo demokrasia wala kugusi ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaoshuhudiwa katika nchi ya Bahrain na Saudi Arabia, alifumbia macho jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na watawala wa nchi hizo mbili huko Yemen na kusifu kile alichosema ni mchango wa Riyadh na Manama katika kuimarisha utulivu!

Matamshi hayo ya Kerry yametolewa katika hali ambayo ni kwa zaidi ya miaka minne sasa ambapo serikali ya kiimla ya Bahrain inaendelea kuwakandamiza wananchi wanaodai haki zao za kimsingi. Maelfu ya raia wa Bahrain wamehukumiwa kifungo jela na wengine kuhukumiwa kifo au kunyang'anywa uraia kwa sababu tu ya kukosoa serikali au kudai haki zao za kidemokrasia. Katika upande mwingine Saudi Arabia, ikitumia silaha za Marekani na Uingereza, inaendelea kuwaua bila ya huruma raia wa Yemen. Pamoja na hayo Marekani inaendelea kuwaunga mkono watawala dhalimu wa nchi hizo mbili. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, nchi hizo zinazotumia fedha nyingi kununua silaha, ni waitifaki wakubwa wa Marekani katika Mashariki ya Kati na zinauona usalama wao katika kuvuruga usalama wa nchi nyingine.