Radiamali mbalimbali kwa madai ya haki za binadamu ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47458-radiamali_mbalimbali_kwa_madai_ya_haki_za_binadamu_ya_marekani
Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameashiria urongo wa madai ya Marekani kuhusiana na haki za binadamu na kusisitiza kuwa, watu wote ulimwenguni wanapaswa kutambua kuwa, Marekani ni dola laghai na haipasi kuamini hata kidogo siasa za Washington.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 15, 2018 06:41 UTC
  • Radiamali mbalimbali kwa madai ya haki za binadamu ya Marekani

Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameashiria urongo wa madai ya Marekani kuhusiana na haki za binadamu na kusisitiza kuwa, watu wote ulimwenguni wanapaswa kutambua kuwa, Marekani ni dola laghai na haipasi kuamini hata kidogo siasa za Washington.

Sheikh Naim Qassim amesema kuwa, inachokifuatilia Marekani si kingine ghairi ya maslahi na manufaa yake na hatua yake ya kuziwekea vikwazo baadhi ya nchi imezidisha mashinikizo kwa wananchi wa mataifa husika.

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameashiria hatua ya Marekani ya kutoguswa hata kidogo na mauaji ya watoto, wanawake na wazeenchini Yemen na kubainisha kwamba, Marekani ni dola la kibeberu ambalo liko nyuma ya pazia ya mauaji na uharibifu mkubwa katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mauaji ya Saudi Arabia dhidi ya watoto wa Yemen yanayofanyika kwa uungaji mkono wa Marekani

Itakumbukwa kuwa, Alkhamisi iliyopita  ndege za kivita za Saudi Arabia zilishambulia basi lililokuwa limebeba wanafunzi katika mji wa Dhahyan, mkoani Sa'ada huko Yemen na kuua wanafunzi 55 na kujeruhi wengine karibu 80. Aktahri ya wahanga hao walikuwa watoto wadogo wenye umri wa chini ya miaka 15 ambao walikuwa wakirejea nyumbani baada ya kuhudhuria masomo ya Qur'ani ya msimu wa joto.

Afisa mmoja katika Wizara ya Ulinzi yya Yemen amefichua kuwa, bomu lililotumika katika shambulio hilo la kikatili la muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia lilitengenezwa Marekani na ni miongoni mwa mabomu ya kuongozwa kwa mbali aina ya MK82.

Ali Murad, mtafiti na mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa nchini Lebanon amesisitiza kuwa, Saudi Arabia imekuwa ikifanya jinai nchini Yemen kwa idhini na baraka kamili za Marekani. Serikali ya Marekani imekuwa ikipinga na kuzuia kufanyika aina yoyote ile ya uchunguzi wa kimataifa hata utakaosimamiwa na timu ya kimataifa ya kutafuta ukweli kuhusiana na jinai za Saudi Arabia dhidi ya raia huko nchini Yemen.

Rais Donald Trump wa Marekani

Ukweli wa mambo ni kuwa, Marekani inafanya unafiki inapoitaka Saudi Arabia eti ifanye uchunguzi kuhusiana na shambulio dhidi ya basi lililokuwa limebeba watoto, kwani kufanya hivyo ni kumtaka mtu aliyetenda jinai afanye uchunguzi kuhusiana na jinai yake hiyo. Bernie Sanders Seneta wa kujitegemea wa Marekani naye amesema katika radiamali yake kwa mashambulio ya anga ya Saudi Arabia na Imarati dhidi ya basi lililokuwa limebeba watoto huko Dhahyan Yemen kwamba: Marekani ni mshirika wa jinai zinazofanyika nchini Yemen kutokana na kuupatia silaha utawala wa Aal Saud na kuandaa mazingira ya ndege za kijeshi za muungano huo wa Kiarabu kupata mafuta na misaada mingine katika operesheni za kijeshi.

Utawala wa Aal Saud kwa idhini na baraka ilizopata kutoka kwa Marekani likiwemo tangazo la Washington la uungaji mkono wa kila upande katika fremu ya misaada ya kijeshi, kiuchumi na kisiasa, umezidisha jinai zake dhidi ya watu wa Yemen. Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Marekani ambayo inadai kuwa ni muungaji mkono na mshika bendera ya demokrasia imekuwa ikitenda dhulma maradufu kutokana na kunyamazia kimya jinai za Saudi Arabia na kuwa kwake pamoja na watawala wa Riyadh katika kukwamisha hatua na juhudi za kuchukuliwa uamuzi wowote ule wa kimataifa za kuifanya Saudia isitishe jinai zake.

Ukiukaji wa haki za binadamu nchini Marekani

Hatua ya Saudi Arabia ya kutumia silaha za kisasa na zenye nguvu kubwa ya uharibifu na ambazo imepatiwa na madola ya Magharibi, imeitumbukiza Yemen katika maafa makubwa zaidi huku maeneo mbalimbali ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu yakifanywa medani ya kujaribia silaha za madola ya Magharibi. 

Radiamali ya fikra za waliowengi ulimwenguni kwa jinai za Saudi Arabia na uungaji mkono wa Marekani kwa jinai hizo, vinabainisha kwamba, siasa za hadaa na ghiliba za Aal-Saud na waungaji mkono wake wa Magharibi haziwezi kufunika na kuficha jinai zinazofanywa na washirika hao dhidi ya wananchi wa Yemen; na ufichuaji wa Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon unaweza kutathminiwa katika uwanja huu.