Umoja wa Mataifa watahadharisha juu ya wimbi jipya la kipindupindu Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47812
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu uwezekano wa kuibuka tena wimbi jipya la maradhi ya kipindupindu nchini Yemen.
(last modified 2025-07-16T07:41:47+00:00 )
Aug 31, 2018 14:07 UTC
  • Umoja wa Mataifa watahadharisha juu ya wimbi jipya la kipindupindu Yemen

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu uwezekano wa kuibuka tena wimbi jipya la maradhi ya kipindupindu nchini Yemen.

Indhari hiyo ya Umoja wa Mataifa imetolewa sambamba na tangazo la Wizara ya Afya ya Yemen kwamba, idadi ya wahanga wa maradhi hayo ya waba imeongezeka na kufikia 73. 

Ripoti zinasema kuwa, kuendelea mashambulio ya kijeshi ya Saudi Arabia nchini Yemen na kuharibiwa miundombinu ya nchi hiyo hususan kanali ya usambazaji maji, kumeyafanya maradhi ya kipindupindu yaenee kwa kasi nchini humo.

Stephane Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa  ameelezea wasiwasi mkubwa uliopo wa kuibuka wimbi la tatu la maradhi ya kipindupindu nchini Yemen na kusema kuwa, umoja huo umesajili kesi 120,000 zinazoshukiwa kuwa ni za maradhi ya kipindupindu nchini humo katika kipindi cha kati ya Januari na Agosti mwaka huu.

Uhaba wa chakula ni moja ya matatizo makubwa yanayowakabili watoto wa Yemen

Mashirika ya utoaji misaada ya kibinadamu yametoa chanjo kwa watu zaidi ya laki nne katika maeneo mbalimbali ya Yemen. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza mara kadhaa kwamba, kiwango cha vifo nchini Yemen vinavyosababishwa na lishe duni kinazidi kuongezeka.

Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi.

Hata hivyo utawala wa Aal Saud na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu nchini humo.