Answarullah: Marekani ndio yenye maamuzi ya kuendelea au kukomeshwa vita Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i49119-answarullah_marekani_ndio_yenye_maamuzi_ya_kuendelea_au_kukomeshwa_vita_yemen
Mjumbe wa Kisiasa wa Harakati ya Answarullah nchini Yemen amesema kuwa, Saudi Arabia na nchi nyingine zilizoivamia nchi hiyo, zinafuata maamuzi ya Marekani katika kuendeleza au kukomeshwa vita vyao vya kichokozi nchini Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 29, 2018 10:24 UTC
  • Answarullah: Marekani ndio yenye maamuzi ya kuendelea au kukomeshwa vita Yemen

Mjumbe wa Kisiasa wa Harakati ya Answarullah nchini Yemen amesema kuwa, Saudi Arabia na nchi nyingine zilizoivamia nchi hiyo, zinafuata maamuzi ya Marekani katika kuendeleza au kukomeshwa vita vyao vya kichokozi nchini Yemen.

Dhaifullah al-Shami ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Al-Alam na kuongeza kwamba, Saudia na washirika wake katika vita vya Yemen ni vibaraka wa Marekani na kwamba msimamo wa wanachama wa muungano vamizi wa Saudia kuhusu mazungumzo yajayo nchini Yemen unategemea maamuzi ya Marekani kwa ajili ya kushiriki mazungumzo hayo. Kiongozi huyo wa Yemen ameendelea kusema kuwa, Saudia ni wenzo wa kutekeleza njama na mipango ya Marekani na utawala haramu wa Israel katika eneo la Mashariki ya Kati.

Dhaifullah al-Shami, Mjumbe wa Kisiasa wa Harakati ya Kiislamu ya Answarullah nchini Yemen 

Al-Shami ameongeza kuwa, ili kukomeshwa mashambulizi ya Saudia nchini Yemen ni lazima kuchukuliwe hatua za kivitendo na kufanyike juhudi za kweli.

Katika hatua nyingine Jumapili ya jana ndege za muungano vamizi wa Saudia zilifanya mashambulizi matano katika eneo la Kilo 16 la mkoa wa Al Hudaydah, magharibi mwa Yemen na mashambulizi manne mengine katika eneo la al-Rusaifat katika viunga vya mji wa Kitaf, mkoa wa Saada, kaskazini mwa nchi hiyo. Mashambulizi hayo yamesababisha hasara na uharibu wa hali na mali.