Kaburi la umati la watu 1500 lagunduliwa Raqqah, Syria
Mkuu wa Chama cha Madaktari mjini Raqqah Syria ametangaza habari ya kugunduliwa kaburi moja la umati lililozikwa watu 1500 mjini humo.
Akihojiwa na gazeti la al Watan la Syria, Jamal al Isa amesema kuwa, kila siku kunagunduliwa jinai kubwa zaidi za magaidi wa Daesh na muungano wa madola ya kigeni yanayoongozwa na Marekani huko kaskazini mashariki mwa Syria.
Amesema, baada ya muungano unaoongozwa na Marekani kuliondoa genge la Daesh huko Raqqah na kulipeleka sehemu nyingine, muungano huo ulianza kuushambulia kikatili na kiholela mji huo na kuuvuruga kabisa licha ya kwamba wakati fulani ulikuwa kimbilio la mamilioni ya watu. Baada ya mashambulizi hayo ya kikatili ya Marekani, asilimia 85 ya mji huo imeharibiwa kikamilifu hivi sasa.
Mkuu wa Chama cha Madaktari wa Raqqah Syria ameongeza kuwa, hadi hivi sasa kumeshagunduliwa miili ya watu elfu nne waliozikwa kwenye makaburi ya umati mjini humo bila ya kuongeza idadi ya watu waliouawa na kuzikwa katika maeneo ya raia ya wakazi wa maeneo hayo.
Marekani, Uingereza na Ufaransa zimefanya jinai kubwa nchini Syria kwa madai ya kupambana na makundi ya kigaidi. Nchi hizo za kibeberu za Magharibi zimeivamia Syria bila ya idhini ya serikali ya nchi hiyo bali hata bila ya idhini ya Umoja wa Mataifa katika hali ambayo ni nchi hizo hizo za Magharibi ndizo zilizoyaunda na kuyapa silaha na mafunzo ya kijeshi magenge ya kigaidi kama Daesh (ISIS) ambayo hivi sasa zinadai kuyapiga vita.