Ndege za Marekani zazidi kuua raia nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i49623-ndege_za_marekani_zazidi_kuua_raia_nchini_yemen
Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa, ndege zisizo na rubani za Marekani zinaendelea kuua raia maskini wa Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 20, 2018 00:12 UTC
  • Ndege za Marekani zazidi kuua raia nchini Yemen

Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa, ndege zisizo na rubani za Marekani zinaendelea kuua raia maskini wa Yemen.

Shirika hilo lilitangaza habari hiyo jana Jumatatu na kuongeza kuwa, idadi ya raia wa Yemen wanaouliwa kwa ndege zisizo na rubani za Marekani imeongezeka sana katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Kwa mujibu wa shirika hilo, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Washington yameongezeka sana nchini Yemen tangu Donald Trump aingie madarakani huko Marekani kiasi kwamba katika kipindi hicho cha miaka miwili pekee, ndege hizo zimefanya mashambulizi yasiyopungua 176 dhidi ya raia wa Yemen.

Hii ni katika hali ambayo, mashambulio yote yaliyofanywa na ndege zisizo na rubani za Marekani katika kipindi chote cha miaka minane cha urais wa Barack Obama yalikuwa ni 154.

Marekani inashiriki katika vita dhidi ya Yemen ikiwa ni pamoja na kuzijazia mafuta angani ndege zinazofanya jinai nchini humo

 

Associated Press limeongeza kuwa, thuluthi nzima ya wahanga wa mashambulio ya ndege za Marekani nchini Yemen ni raia wa kawaida wakiwemo watoto wadogo.

Kwa kawaida jeshi la Marekani huwa halizungumzii mashambulizi ya ndege zake zisizo na rubani na hasara zinazosababishwa na ndege hizo huko Yemen lakini baadhi ya familia za wananchi wa Yemen zimeliambia shirika la habari la Associated Press kuwa wamekuwa wakipoteza jamaa zao wengi kutokana na mashambulio ya ndege hizo za Marekani. 

Mashambulizi hayo ya ndege za Marekani yanaendeleo huko Yemen katika hali ambayo Washington ni mmoja wa wadhamini wakuu wa silaha zinazotumiwa na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu  kufanya mashambulizi ya kikatili dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Yemen.