HRW: Saudia haiaminiki tena baada ya kudanganya kuhusu mauaji ya Khashoggi
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeutaka utawala wa Riyadh kuwaruhusu waangalizi huru kutathmini hali ya wanaharakati wanawake wanaozuiliwa katika jela za utawala huo wa kifalme, likisisitiza kuwa Saudi Arabia haiaminiki tena baada ya kutoa taarifa kadhaa za urongo kuhusu mauaji ya Jamal Khashoggi.
Naibu Mkurugenzi wa shirika hilo katika eneo la Mashariki ya Kati, Michael Page amesema kukanusha na kutoa taarifa za urongo Saudia kuhusu mauaji ya Khashoggi kunafanya kauli ya Riyadh kuwa wanarakati wanawake nchini humo hawateswi wakiwa kizuizini itiliwe shaka.
Khashoggi, aliyewahi kuwa msiri na mwandani wa aila ya kifalme inayotawala nchini Saudi Arabia, lakini hatimaye akageuka kuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal Saud, aliuliwa na mwili wake kukatwa vipande vipande, alipoingia kwenye jengo la ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki mnamo tarehe Pili Oktoba mwaka huu.
Awali utawala wa Riyadh ulikanusha kuwa ulikuwa na habari kuhusu mahala alipo Khashoggi lakini baadaye ulikiri kwamba, maafisa wake ndio waliomuua mwandishi huyo wa bahari na kumkata vipande vipande.
Human Rights Watch imesema Saudia inapaswa kuwaruhusu waangalizi huru wa kimataifa kukutana na wanawake watetezi za haki za binadamu inaowazuilia tangu Mei mwaka huu, ili wajitathminie wenyewe hali zao na usalama wao.
Novemba 23 Saudia ilipinga vielelezo vilivyochapishwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch Amnesty International vinavyoonesha kuwa maafisa usalama wa Aal-Saud wanawakandamiza na hata kuwadhalilisha kingono wanaharakati wanawake wanaozuiliwa.
Inaarifiwa kuwa, Saud al-Qahtani, aliyekuwa mkuu wa masuala ya vyombo vya habari nchini Saudia na mpambe wa karibu wa Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, kipindi kimoja alishuhudia binafsi mmoja wa wanawake hao akidhalilishwa kingono.