Mahmoud Abbas: Trump anapaswa aheshimu maazimio ya Umoja wa Mataifa
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameitaka serikali ya Marekani iheshimu maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina.
Mahmoud Abbas aliyasema hayo jana katika sherehe ya kuadhimisha kuzaliwa Nabii Isa Masih (as) iliyofanyika huko Bait Lahm, Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Alisema: Maamuzi aliyochukua Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu Palestina na hasa kuitambua rasmi Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, kukata misaada ya fedha kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa ajili ya Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) na vilevile kusaidia ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni hayakubaliki.
Abbas amesisitiza kuwa, misimamo hiyo ya Trump inapingana na sheria za kimataifa na akaongezea kwa kusema: Washington inapaswa iheshimu maazimio ya Umoja wa Mataifa na kuamiliana na Wapalestina kwa uadilifu.
Kufuatia uamuzi wa Marekani wa kuuhamishia Baitul Muqaddas ubalozi wake uliokuweko Tel Aviv, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alisisitiza kwamba: Hatokubali usuluhishi wowote wa Washington katika mchakato wa mazungumzo ya mapatano baina ya pande mbili za Wapalestina na Wazayuni.
Itakumbukwa kuwa, tarehe 12 Desemba mwaka uliopita wa 2017, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio lilioungwa mkono kwa kura 128 na kupingwa kwa kura tisa tu za nchi wanachama, ambalo lililaani hatua ya Marekani ya kuuhamishia ubalozi wake katika mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem).../