EU, Amnesty zaikosoa Bahrain kwa kumfunga maisha jela Sheikh Salman
Umoja wa Ulaya umekosoa vikali hatua ya Mahakama ya Juu ya Bahrain ya kuidhinisha kifungo cha maisha jela dhidi ya shakshia mashuhuri wa kidini na kisiasa nchini humo, Sheikh Ali Salman.
Katika taarifa, EU imesema kitendo hicho ni hatua nyingine mbele ya utawala wa Manama ya kuzinyamazisha sauti za wapinzani, na kwamba uamuzi huo utafifiza uwezekano mdogo uliokuwepo wa kufanyika mazungumzo ya kisiasa yatakayozijimuisha pande zote husika.
Taarifa hiyo ya Umoja wa Ulaya kadhalika imeeleza wasiwasi wa Brussels wa kushadidi mbinyo dhidi ya wapinzani na wakosoaji wa serikali nchini Bahrain.
Kadhalika shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeutaja uamuzi huo wa vyombo vya mahakama vya Manama kuwa pigo jingine kwa uhuru wa kujieleza nchini Bahrain.
Hapo jana Jumatatu, mahakama hiyo ilifanya kikao na kuidhinisha hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa Sheikh Ali Salman, mwanazuoni mashuhuri wa Bahrain ambaye alikuwa akikabiliwa na tuhuma zisizo na msingi za eti kuifanyia ujasusi Qatar.

Tarehe 24 Oktoba mwaka jana utawala wa kiukoo wa Aal-Khalifa uliwapokonya uraia Sheikh Ali Salman ambaye ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya al Wifaq, pamoja na Hassan Sultan na Ali al Aswad, wabunge wawili wa zamani wa bunge la Bahrain kwa tuhuma zisizo na msingi kwamba walikuwa wakiifanyia ujasusi Qatar na kisha ikawahukumu kifungo cha maisha.
Utawala wa Aal Khalifa umechukua hatua hiyo katika hali ambayo Jumuiya ya Kiislamu ya al Wifaq imetangaza katika taarifa yake kuwa, jumuiya hiyo tayari ilikuwa imeshatoa ushahidi na kuwasilisha mahakamani nyaraka zenye hoja madhubuti za kupinga tuhuma hizo.