Jeshi la Saudia laua raia watano katika eneo la Qatif
(last modified Sun, 03 Feb 2019 15:55:39 GMT )
Feb 03, 2019 15:55 UTC
  • Jeshi la Saudia laua raia watano katika eneo la Qatif

Jeshi la Saudi Arabia limehujumu mji WA Qatif katika mkoa wa Ash-Sharqiyyah na kuua raia watano na kuwajeruhi wengine kadhaa.

Televisheni ya Al Manar imeripoti kuwa, siku ya Jumamosi, askari wa Jeshi la Saudia waliyavamia na kuyazingira maeneo ya Umul Hamam na Al Jash mjini Qatif na kuua watu watano na kujeruhi wengine kadhaa. Aidha raia kadhaa wamekamatwa katika msako huo wa askari wa utawala wa kiimla wa Saudi Arabia.

Disemba 9 mwaka jana pia, wanajeshi wa Saudia walihujumu maeneo kadhaa ya mji wa Qatif, ambao wakazi wake wengi ni Waislamu wa Kishia,  na kuua raia watano na kujeruhi wengine wawili.

Mji wa Qatif umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara na wanajeshi wa Saudi Arabia na hadi sasa mamia ya wakazi wa mji huo wameuawa na wengine wengi kukamatwa kutokana na harakati zao za kisiasa.

Eneo la mashariki mwa Saudi Arabia tokea mwaka 2011 limekuwa medani ya maandamano ya wananchi wanaolalamikia udhalimu wa utawala wa ukoo wa Aal Saud hasa ukadamizaji na ukosefu wa uadilifu katika kugawa utajiri wa nchi.

Itakumbukuwa kuwa eneo hilo la mashariki mwa Saudia ndilo lenye utajiri mkubwa zaidi wa mafuta nchini humo lakini wakazi wa eneo hilo, ambao aghalabu ni Waislamu wa madhehebu ya Shia, wamekuwa wakikandamizwa na kudhulumiwa kwa muda mrefu sana.