Wafanyabiashara wa Kipalestina wasusia mkutano wa Trump, Bahrain
Wafanyabiashara na wawekezaji mashuhuri wa Kipalestina wametangaza bayana kuwa hawatoshiriki mkutano wa 'kiuchumi wa Manama' nchini Bahrain ulioitishwa na Marekani, wenye lengo la kuzindua 'Muamala wa Karne', wakisisitiza kuwa kile ambacho Wapalestina wanahitajia ni uhuru wao na wala sio fedha.
Baadhi ya wawekezaji hao wa Kipalestina waliopokea mualiko wa Marekani wa kushiriki mkutano huo ni Murad Tahboub, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la teknolojia la ASAL, ambaye amesema: "Kadhia yetu ni ya kisiasa kwa asilimia 100, na wala sio ya kiuchumi."
Mjasiriamali mwingine mashuhuri wa Kipalestina ambaye ametangaza kuwa hatoshiki mkutano huo wa Manama licha ya kupokea barua ya mualiko kutoka Wizara ya Hazina ya Marekani ni Ammar Aker, Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika la mawasiliano la Paltel, ambalo linahesabiwa kuwa muajiri mkubwa zaidi wa kibinafsi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.
Amesema mazungumzo ya kisiasa na diplomasia kwa shabaha ya kuundwa taifa huru la Palestina ndiyo njia pekee ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Palestina na utawala haramu wa Israel.
Mkutano huo ulioitishwa na Marekani umepangwa kufanyika tarehe 25 na 26 za mwezi huu ambapo katika jukwaa hilo kutatangazwa nara bandia ya 'kuvutia uwekezaji na eti kuboresha hali ya kiuchumi ya Wapalestina' katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza ambao nao uko chini ya mzingiro.
Mpango wa Muamala wa Karne ambao unadaiwa na Wamarekani kuwa utahitimisha mzozo wa Wapalestina na Wazayuni, mbali na kufuta kabisa ndoto ya kurejea makwao wakimbizi wa Kipalestina, unawazuia pia kuunda nchi yao huru sambamba na kubariki rasmi uvamizi wa utawala wa Kizayuni na kuufanya uendelee kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.