Russia yaunga mkono njia ya kuutatua kisiasa mgogoro wa Syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amehimiza kufanyika juhudi zaidi za kuutatua kisiasa mgogoro wa Syria na kujiepusha na kutumia mabavu.
Sergey Lavrov alitoa mwito huo jana (Ijumaa) wakati alipoonana na Geir Pedersen, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria na kuongeza kuwa, ubunifu wa nchi tatu za Russia, Iran na Uturuki wa kutatua kwa njia za amani mgogoro wa Syria maarufu kwa jina la "Mazungumzo ya Astana," umezaa matunda tab'an kwa kushirikiana kikamilifu na Umoja wa Mataifa.
Ameongeza kuwa, Russia, Uturuki na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinaendeleza juhudi zao za kutafuta suluhisho la kudumu la amani la mgogoro wa Syria.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Russia ametilia mkazo pia wajibu wa kusafishwa na kuangamizwa ugaidi huko Syria na wakati huo huo kutafutwa njia za kisiasa za kutatua mgogoro wa nchi hiyo kwa mujibu wa azimio nambari 2254 la Umoja wa Mataifa.
Kwa upande wake, Geir Pedersen, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria amesema kuwa, umoja huo unaunga mkono juhudi za kuutatua kisiasa mgogoro wa nchi hiyo na unapinga kutumiwa nguvu za kijeshi.
Vile vile amesema, Kamati ya Katiba ya Syria ni mlango wa kuingilia kwenye utatuzi wa kudumu wa mgogoro wa nchi hiyo na kwamba pande husika zimeshakaribia kumaliza zoezi la kuunda kamati hiyo.