Ujerumani yakataa ombi la Marekani la kutuma askari Syria
Rais Donald Trump wa Marekani Disemba mwaka 2018 aliwaahidi Wamarekani kwamba ataliondoa jeshi la nchi hiyo huko Syria. Trump alitoa ahadi hiyo katika kile kinachoaminika kuwa ni sehemu ya kutekeleza kampeni yakee ya kubakia ikulu ya White House.
Hata hivyo kiongozi huyo amebadilisha mtazamo wake katika uwanja huo na sasa Washington inafanya jitihada za kuwaburuta washirika wake huko Syria japo kuwa suala hilo limepingwa vikali. Katika uwanja huo serikali ya Ujerumani imepinga ombi la Marekani la kutuma askari wake huko Syria kushiriki katika kile kinachoitwa muungano wa kukabiliana na Daesh. Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Steffen Seibert amewaambia waandishi habari kwamba, nchi hiyo haitatuma askari yeyote katika ardhi ya Syria na haitabadilisha msimamo huo.
Seibert amesema kuwa Ujerumani inashirikiana na Marekani katika baadhi ya masuala madogo huko Syria na kuongeza kuwa: "Hata hivyo Berlin inapinga suala la kutuma wanajeshi wa Kijerumani huko Syria kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, na iwapo itaamua kuendeleza hatua zake katika fremu ya muungano wa kukabiliana na Daesh, basi hatua hizo hazitajumuisha suala la kutuma wanajeshi wa nchi kavu huko Syria."
Hatua hiyo imechukuliwa na Berlin baada ya Marekani kuitaka Ujerumani itume wanajeshi nchini Syria. Mwakilishi maalumu wa Rais wa Marekani katika masuala ya Syria, James Jeffrey ambaye aliitembelea Ujerumani hivi karibuni aliitaka Berlin ishirikiane na Marekani kwa kutuma kikosi cha jeshi nchini Syria. Jeffrey alisema Washington inataka askari wa Ujerumani wachukue nafasi ya wenzao wa Marekani nchini Syria na Washingrton inatarajia kwamba, Berlin itakubaliana na ombi hilo.
Ombi hilo la Marekani imekataliwa na serikali ya Ujerumani na vya vyama vya upinzani. Gazeti la Die Welt liliandika katika toleo lake la jana Jumatatu kwamba: Muungano wa vyama tawala na kambi ya upinzani umepinga vikali ombi hilo la Marekani.
Marekani ambayo ni kinara wa nchi za Magharibi ndiye muungaji mkono na mfadhili mkuu wa makundi ya kigaidi huko Syria, inaendelea kuwepo kinyume cha sheria katika ardhi ya nchi hiyo kwa kisingizio cha kupamba na kundi la Daesh. Baada ya kutangazwa uamuzi wa Donald Trump wa kuliondoa jeshi la Marekani katika ardhi ya Syria ili kutimiza ahadi alizotoa katika kampeni za uchaguzi, maafisa wa nchi hiyo wakiwemo wabunge walikosoa vikali uamuzi huo. Kwa msingi huo Tramp alibadilisha uamuzi huo kutokana na mashinikizo ya ndani na kutoka kwa waitifaki wake wa Ulaya na kurefusha kipindi cha kuondoka askari wa Marekani kutoka siku 30 hadi siku 120. Vilevile alilazimia kubadili misimamo yake jumla kuhusiana na Syria. Katika hotuba yake ya tarehe Pili Januari Trump alidai kuwa hata baada ya kuondoka askari wa Marekani nchini Syria lakini Washington itaendelea kuwalinda Wakurdi wa nchi hiyo. Kwa msingi huo Marekani inang'ang'ania kubakisha wanajeshi wake katika ardhi ya Syria kwa kisingizio cha kuwalinda Wakurdi wa nchi hiyo. Sasa Washington inaitaka Berlin ikubali kugawana majukumu na nchi hiyo na kupunguza mashinikizo kwa askari wake walioko kaskazini mwa Syria kwa kutuma askari nchini humo.
Hata hivyo Wajerumani wanajua vyema kwamba, siasa za nchi za Magharibi za kuyaunga mkono makundi ya kigaidi kwa malengo yao makhsusi ikiwa ni pamoja na kuindoa madarakani serikali halali ya Bashar Assad zimeshindwa na kufeli na makundi hayo yameshindwa na yamo katika hali ya kusambaratika kabisa. Wajerumani wanaamini kwamba, kutuma wanajeshi nchini Syria ni sawa na kushiriki katika mchezo uliofeli na kushindwa na Marekani nchini humo.
Syria imekuwa ikitangaza mara kwa mara kwamba kuwepo kwa wanajeshi wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo ni kinyume cha sheria. Kwa msingi huo Moscow na Damascus zimeutaka Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa zichukue msimamo mmoja na kuitaka Marekani iondoe wanajeshi wake katika ardhi ya Syria haraka iwezekanavyo.