Pakistan: Tupo tayari kufanya mazungumzo na India
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan amesema kuwa Islamabad ipo tayari kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya amani na India.
Mohammad Faisal, ameyasema hayo katika kikao na waandishi wa habari mjini Islamabad na kusema kuwa, Pakistan inakaribisha upatanishi wa Marekani kwa ajili ya kutatua mzozo wa eneo la Kashmir. Faisal ameongeza kwamba, licha ya askari wa India kuendeleza ufyatuaji risasi katika eneo la mpaka wa pamoja, lakini Pakistan imejiandaa kwa ajili ya kutatuliwa mzozo huo kwa njia ya mazungumzo. Tangu siku ya Jumatatu iliyopita, askari wa India na Pakistan wameanzisha duru mpya ya mashambulizi katika mpaka huo wa pamoja.
Askari hao wa nchi mbili wamekuwa wakituhumiana kwa ukiukaji wa makubaliano ya usitishaji vita katika mpaka wa eneo la Kashmir. Inafaa kuashiria kuwa India na Pakistan zilitiliana saini makubaliano ya usitishaji vita mwaka 2003 katika eneo la Kashmir, hata hivyo tangu wakati huo nchi hizo zimekuwa zikiyakiuka makubaliano hayo mara kwa mara. Kashmir ni moja ya maudhui muhimu ambazo nchi mbili zinatofautiana juu yake ambapo kila mmoja anadai umiliki wake.