Benjamin Netanyahu katika ukingo wa kuporomoka
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i56119-benjamin_netanyahu_katika_ukingo_wa_kuporomoka
Zaidi ya asilimia 90 ya kura zilizohesabiwa katika uchaguzi wa bunge la utawala haramu wa Israel, inaeleza kuwa Benjamin Netanyahu yuko katika ukingo wa kutupwa kando, na kuna uwezekano wa kuingia madarakani waziri mkuu mpya.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Sep 20, 2019 02:25 UTC
  • Benjamin Netanyahu katika ukingo wa kuporomoka

Zaidi ya asilimia 90 ya kura zilizohesabiwa katika uchaguzi wa bunge la utawala haramu wa Israel, inaeleza kuwa Benjamin Netanyahu yuko katika ukingo wa kutupwa kando, na kuna uwezekano wa kuingia madarakani waziri mkuu mpya.

Uchaguzi wa pili wa bunge la utawala wa Kizayuni katika kipindi cha miezi sita ya hivi karibuni, ulifanyika Jumanne iliyopita ya tarehe 17 ya mwezi huu. Hadi sasa matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo, bado hayajatangazwa, ingawa takwimu zilizotolewa zinaeleza kupungua viti vya chama cha Likud, na kuangukia pua Benjamin Netanyahu. Uchaguzi huo ulitofautiana na uchaguzi kama huo uliofanyika tarehe 9 Aprili mwaka huu. Hii ni kusema kuwa katika uchaguzi wa mwezi Aprili, chama cha Likud kilipata viti 36, huku muungano wa Blu na Nyeupe, ukipata viti 35. Hata hivyo katika uchaguzi wa Jumanne na kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa, chama cha Likud kimepata viti 32, huku muungano wa Blu na Nyeupe (yaani Blue and White alliance) ukipata viti 33, suala ambalo linaonyesha kuwa mirengo yote miwili imezidi kuporomoka. Nukta muhimu ni hii kwamba, gazeti la lugha ya Kiebrania la Yodiot Aharont limeandika kuwa, kura kilizopata chama cha Likud katika vitongozi vya walowezi wa Kizayuni vinavyopakana na Ukanda wa Gaza, zimepungua.

Kupenda vita kwa Benjamin Netanyahu, kumeyagharimu maisha yake ya kisiasa ndani ya Israel

Na hii ni kwa kuwa wakazi wa maeneo hayo hawafurahishwi na ongezeko la mizozo na kuzorota kwa hali ya usalama katika maeneo tajwa. Kwa maneno mengine ni kwamba, hatua ya kupenda vita ya Benjamin Netanyahu, imekuwa na matokeo kinyume na hasi kwa waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni na chama chake cha Likud. Raia wa Israel si tu kwamba wanaamini kuwa Netanyahu hawezi kuwadhaminia usalama, bali wanamtambua kiongozi huyo kuwa ni chanzo cha kuibuka ghasia na machafuko. Tofauti nyingine katika metokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni na uchaguzi wa tarehe tisa Aprili ni hii kwamba, kura za muungano wa pamoja wa Kiarabu zimeongezeka, na hii ni kwa kuwa kiwango cha ushiriki wa Waarabu wanaoishi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu katika uchaguzi uliopita kiliongezeka kutoka asilimia 50 hadi asilimia 60.  Kwa matokeo hayo, muungano wa pamoja wa Kiarabu, umetajwa kuwa mrengo wa tatu wa kisiasa ndani ya Israel. Kuhusiana na suala hilo Ayman Odeh, kiongozi wa mrengo huo na ambaye pia ni mwanasheria anasema: "Matokeo ya awali ya uchaguzi yanaonyesha kwamba Waarabuu ni kizuizi cha kuundwa serikali ya mrengo wa kulia wenye kufurutu ada chini ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu." Ama nukta nyingine ni kwamba, kura za chama cha Yisrael Beiteinu kinachoongozwa na Avigdor Lieberman, nazo zimeongezeka, katika hali ambayo mwanasiasa huyo ndiye muhusika mkuu wa kusambaratika kwa baraza la mawaziri la Netanyahu hapo Novemba mwaka jana. Aidha Avigdor Lieberman ndiye muhusika mkuu wa kufeli mchakato wa kuundwa baraza jipya baada ya uchaguzi wa Aprili.

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa utawala wa Kizayuni

Hivi sasa pia Lieberman ametangaza kuwa iwapo Netanyahu atapewa jukumu la kuunda serikali, basi hatokubali kuungana na waziri mkuu huyo. Hii ikiwa na maana kwamba iwapo Netanyahu atatakiwa aunde serikali, hatafanikiwa kuunda muungano ndani ya Israel. Hali hiyo inamaanisha kwamba Netanyahu yuko katika ukingo wa kuporomoka kisiasa. Kwa upande mwingine ni kwamba huenda Benjamin Netanyahu asipewe idhini na rais wa utawala wa Kizayuni ya kuunda serikali. Iwapo hali hiyo itatokea, ni wazi kuwa kiongozi huyo atatupwa jela kutokana na mafaili manne ya ufisadi yanayomkabili. Aidha kwa upande mwingine ni kwamba, hata kama Netanyahu atapewa idhini ya kuunda serikali kutokana na matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni, kuna uwezekano mkubwa wa kukumbwa na mazingira magumu kuliko yale ya mwezi Aprili na Mei mwaka huu na hivyo kushindwa tena katika juhudi zake za kuunda serikali mpya ya utawala huo.